Bondi ya jamaa aliyeshtakiwa kwa kuiba nyama 181kgs yapunguzwa kutoka Sh10m hadi Sh150k

Jamaa huyo alishtakiwa kwa kuingia kwenye klabu moja ya starehe wakati wa maandamano na kuiba mitungi ya gesi, viti, kochi la mgahawa, vyombo, vyakula, mkaa, kilo 181 za nyama ya ng’ombe, miongoni mwa vitu vingine.

Muhtasari

• Paul Mutua alifikishwa katika mahakama mjini humo na kushtakiwa kwa visa vya uhalifu wa mali na wizi wakati wa maandamano ya wiki jana ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

• Jumanne, mahakama ilimuachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 10, jambo ambalo lilizua vilio na malalamiko mengi kutoka kwa umma.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Baada ya kilio kingi kutoka kwa umma kuhusu dhamana aliyoachiliwa jamaa mmoja anayeshukiwa kwa wizi wa nyama na vitu vingine mjini Eldoret, mahakama kuu sasa imeingilia kati na kupunguza dhamana hiyo.

Paul Mutua alifikishwa katika mahakama mjini humo na kushtakiwa kwa visa vya uhalifu wa mali na wizi wakati wa maandamano ya wiki jana ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Jumanne, mahakama ilimuachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 10, jambo ambalo lilizua vilio na malalamiko mengi kutoka kwa umma.

Mawakili wa Azimio wakiongozwa na mwanasiasa Babu Owino waliingilia kati na kuandikia mahakama kuu ya Eldoret barua wakitaka dhamana ya Mutua kuangaziwa upya.

"Kupitia kwa Wakili wetu Aseso Omollo tulitafuta Mapitio ya masharti ya bondi kutoka kwa shilingi milioni 10 ambayo aliwekewa Jonathan Mutua kwa madai ya kuiba kilo 181 za Nyama huko Eldoret hadi dhamana ya pesa taslimu ya shilingi 150K," alifichua MP Babu Owino.

Mahakama, ilipokagua Jumatano, ilimwachilia mshukiwa kwa dhamana ya pesa taslimu Ksh.200,000, kwa chaguo la bondi ya Ksh.150,000

Alishtakiwa kwa kuingia katika Ukumbi wa Baniyas Club Square unaomilikiwa na kuiba vitu vya thamani ya Ksh.37,093,690.

Vitu vilivyoibiwa ni pamoja na skrini za televisheni, kompyuta, printa, mitungi ya gesi, viti, kochi la mgahawa, vyombo, vyakula, mkaa, kilo 181 za nyama ya ng’ombe, magunia 17 ya mkaa na magunia 12 ya viazi.

Mutua, 29, hata hivyo alikanusha mashtaka hayo alipofika mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Cherono Kesse. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Julai 15, 2024.