MICHUANO YA EURO 2020

Euro 2020: Fahamu wachezaji ambao wana asili ya ukanda wa Afrika Mashariki

Wako wachezaji 55 wenye asili ya Afrika wanaowakilisha mataifa ya Ulaya.

Muhtasari

•Timu ya taifa ya Ufaransa ina wachezaji 12 wenye asili ya Afrika akiwemo Ngolo Kante mwenye asili ya Mali, Kylian Mbappe (Cameroon) Karim Benzema (Algeria) na Paul Pogba (Guinea), Huku Finland na Ujerumani zikiwa na wachezaji wengi pia weye asili ya Afrika. Mfano Ujerumani ina Antonio Rudiger (Sierra Leone), Serge Gnabry (Ivory Coast), Jamal Musiala (Nigeria) na Leroy Sane, ambaye baba yake aliwahi kucheza ligi ya Ujerumani ana asili ya Senegal.

GOAL

Mashindano ya Euro 2020 yanaendelea katika mjiji 11 barani Ulaya, ni mashindano yanayoshirikisha wachezaji 622 kutoka mataifa 24 barani humo. Kizuri kati ya wachezaji hawa, wako wachezaji 55 wenye asili ya Afrika wanaowakilisha mataifa ya Ulaya.

Timu ya taifa ya Ufaransa ina wachezaji 12 wenye asili ya Afrika akiwemo Ngolo Kante mwenye asili ya Mali, Kylian Mbappe (Cameroon) Karim Benzema (Algeria) na Paul Pogba (Guinea), Huku Finland na Ujerumani zikiwa na wachezaji wengi pia weye asili ya Afrika. Mfano Ujerumani ina Antonio Rudiger (Sierra Leone), Serge Gnabry (Ivory Coast), Jamal Musiala (Nigeria) na Leroy Sane, ambaye baba yake aliwahi kucheza ligi ya Ujerumani ana asili ya Senegal.

Ukiacha hao na wengine maarufu kama David Alaba nahodha wa Austria mwenye asili ya Nigeria, Bukayo Saka (England & Nigeria) na Memphis Depay&Ghana), nchi za ukanda wa Afrika Mashariki nazo hazijaachwa nyuma, walau na zenyewe zina wachezaji kadhaa wanaochezea mataifa ya Ulaya kwenye michuano ya EURO mwaka huu.

Wachezaji hawa ni wale waliozaliwa Afrika wakaenda Ulaya wakiwa wangali wadogo, ama walioasiliwa na raia wa mataifa ya Ulaya, waliozaliwa Ulaya kwa wazazi waafrika kwenye makambi ya wakimbizi ama wazazi walikuwa Ulaya kutafuta maisha na wengine wamezaliwa na mzazi mmoja akiwa mwenye asili ya Afrika na mwingine ni kutoka Ulaya.

DR Congo ambayo imeomba rasmi kujiunga na Jumuia ya Afrika Mashariki inaweza kujivunia kutoa wachezaji wengi wenye asili ya nchi hiyo wanaokipiga kwenye michuano ya Euro mwaka huu.

Mfano mkubwa ni wachezaji kama Steve Mandanda (Ufaransa), Michy Batshuayi na Christian Benteke (Ubelgiji) na Kelvin Mbabu (Switzerland). Ukiacha hawa wafuato ni wachezaji wenye asili ya Afrika Mashariki wanaozibeba zaidi timu zao kwenye michuano ya EURO 2020.

1: Yussuf Polsen (Tanzania & Sweden)

Yusuf
Yusuf
Image: Twitter

Yussuf ana asili ya Tanzania, baba yake Shihe Yurary anatokea mkoa wa Tanga, alikuwa mfanyakazi katika meli za kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na Denmark. Kwenye hizo safari akakutana na Lene Poulsen katika miaka ya 1990's na kuingia kwenye mahusiano na kuzaliwa Yusuf mwaka 1994. Inaelezwa Shihe alifariki kwa maradhi ya kansa wakati Yussuf akiwa na miaka 6 tu.

Katika michuano ya Euro, Yussuf anaibeba Denmark. Yussuf ndiye mchezaji mwenye asili ya Afrika aliyefunga bao la mapema zaidi katika Michuano ya Euro likiwa ni la tatu katika historia ya michano hiyo, kwa magoli yaliyofungwa mapema. Akifunga dakika ya kwanza na sekunde 39 tu dhidi ya Ubelgiji.

Aliwahi kutembelea kwao Tanga kwa bibi yake mara kadhaa mwaka 1996, 2002, 2008 na 2011. Aliyoulizwa kwa nini kaichagua Denmark na si Tanzania Yussuf alisema, 'Kiukweli sikupokea ofa kutoka Tanzania ya kucheza timu ya taifa lakini pia sijui ingekuwaje kama ofa ingekuja', Akirejea uamuzi mgumu wa kuchagua kwa sababu ameshachezea timu za vijana za taifa la Denmark huko nyuma.

2: Romelu Lukaku (DR Congo & Ubelgiji)

Lukaku
Lukaku
Image: Hisani

Lukaku ametoka kuisaidia Inter Milan kutwaa taji la ligi kuu ya Italia (Seria A) kwa kupachika mabao 24, sasa anaibeba Ubelgiji kwenye michuano ya Euro mwaka huu. Amefunga mabao 3 katika hatua ya makundi akitarajiwa kufanya vyema Zaidi kwenye hatua za mtoano.

Kwa soka lake ameshatwaa zawadi ya mchezaji bora wa mechi katika michezo miwili ya Euro shidi ya Urusi ambayo ubelgiji ilishinda 3-0 dhidi ya Denmark walioshinda 2-1. Lukaku mshambuliaji wa zamani wa Manchester United ana asili ya DR Congo,ndiye mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwenye EURO kwa wale wenye asili ya Afrika.

3: Presnel Kimpembe (DR Congo & Ufarasa)

Kipembe
Kipembe
Image: Hisani

Nyota mwingine mweye asili ya DR Congo, anayechezea Ufaransa. Amewahi kuichezea timu ya taifa ya vijana ya DR Congo chini ya miaka 20 mchezo mmoja mwaka 2014, lakini baadaye akaamua kubeba bendera ya Ufaransa badala ya ndugu zake wa DR Congo.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichotwaa kombe la dunia mwaka 2018, na tangu wakati huo avae jezi za Ufaransa ameendelea kuimarika na kuwa miongoni mwa walinzi bora wa kati wanaotumika.

Amezaliwa Ufaransa baba akiwa mcongo na mama kutoka Haiti na mara baada ya kuzaliwa akapewa jina la babu yake kama ilivyo kwa waafrika wengi kwenye kurithi majina ya babu na bibi.

4: Alexander Isak (Eritrea & Sweden)

Isak (kulia) akikabidhiwa jezi ya timu ya taifa ya Eritrea alipoitembelea nchi hiyo.
Isak (kulia) akikabidhiwa jezi ya timu ya taifa ya Eritrea alipoitembelea nchi hiyo.
Image: Hisani

Kijana huyu anawindwa sasa na vilabu vikubwa vikiwemo Manchester United, Arsenal na Atletico Madrid. Uwezo wake unafananishwa na Zlatan Ibrahimovic, gwiji la Sweden na mshabuliaji hatari kuwahi kuchezea vilabu vikubwa kama Inter Milan, AC Milan, Juventus, Barcelona, Ajax, Manchester United na PSG ya Ufaransa.

Isak akiwa na Sweden kwenye Euro ndiye anayevaa viatu vya Zlatan kwenye eneo la ushambuliaji. Kinda huyu mwenye umri wa miaka 21 anayekipigia Real Sociedad na aliyeifungia timu hiyo mabao 33 katika misimu miwili ya ligi kuu ya Hispania (Laliga), anatoka kwa wazazi wenye asili ya Eritrea.

Aliwahi kumfundisha lugha ya tigirinya inayozungumzwa Eritrea nyota mwingine mwenye asili ya Eritrea aliyezaliwa Sweden, Henok Goitom. Hakuwa anajua lugha hiyo, na alipaswa kuwa sehemu ya kikosi cha Eritrea, ili kujumuika vyema baba yake Isak alimfundisha lugha hiyo ya asili.

Mara kadhaa Isak amekuwa akienda kwao Eritrea.

5: Denis Zakaria (Uswisi & Sudan Kusini )

Zakaria (mbele) akiwajibika katika moja ya mechi za timu ya taifa ya Uswiswi
Zakaria (mbele) akiwajibika katika moja ya mechi za timu ya taifa ya Uswiswi
Image: Hisani

Zakaria amezaliwa jijini Geneva, Uswisi, kwa mama kutoka DR Congo na baba kutoka Sudan Kusini.

Anaitwa Denis Lemi Zakaria Lako Lado, kiungo mkabaji wa klabu ya Borussia Monchengladbach anayekipigia timu ya taifa ya Uswiswi. Tayari ameshacheza michezo zaidi ya 30 akiwa na timu hiyo ya taifa, bado hajapata nafasi ya kutosha kuonesha cheche zake kwenye michuano ya Euro ya mwaka huu, lakini ni miongoni mwa wachezaji wazuri wenye asili ya Afrika wanaowakilisha katika Euro 2020.

(Maongezi; Samuel Maina)