Maafisa waliohusishwa na kifo cha ndugu wawili Embu wamesimamishwa kazi - IG Mutyambai

Mutyambai amesema kuwa idara ya IPOA imekamilisha uchunguzi na kupitisha ripoti yake kwa DPP ili hatua zaidi ichukuliwe.

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai amesema kuwa maafisa hao wamesimamishwa kazi ili kupatia nafasi kushtakiwa kwao.

• Bosi huyo wa polisi amehakikishia Wakenya kuwa haki ya ndugu wawili, Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19), itapatikana.

Marehemu Benson Njiru na Emmanuel Mutura
Marehemu Benson Njiru na Emmanuel Mutura
Image: AMNESTY KENYA

Maafisa wa polisi ambao wamehusishwa na kifo cha ndugu wawili waliofariki katika hali tatanishi mnamo  Agosti 1 wamesimamishwa kazi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai amesema kuwa maafisa hao wamesimamishwa kazi ili kupatia nafasi kushtakiwa kwao.

Mutyambai amesema kuwa idara ya IPOA imekamilisha uchunguzi na kupitisha ripoti yake kwa DPP ili hatua zaidi ichukuliwe.

"IPOA imekamilisha upelelezi wake kuhusiana na kesi hiyo na kupitisha ripoti yake kwa DPP kwa hatua zaidi kuchukuliwa. Kwa wakati huo, maafisa wote wamesimamishwa kazi mara moja ili kuruhusu washtakiwe" Mutyambai alisema.

 Bosi huyo wa polisi amehakikishia Wakenya kuwa haki ya ndugu wawili, Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19), itapatikana.

Hata hivyo Mutyambai amewaomba wananchi kuwa watulivu na kusubiri sheria kuchukua mkondo wake.

"Nawahakikishia kuwa haki itapatikana kwa ndugu wawili kutoka KIanjokoma. Lakini hii inaweza fanyika pindi tu tukikubali sheria kufuatwa na kuwepo kwa ushahidi wa kutosha utakaowezesha kesi kuendelea mahakamani" Alisewa Mutyambai.

Mutyambai alifariji familia ya marehemu na kusema kuwa maafisa wa  DCI wamehusishwa kabisa katika upelelezi.

Njiru na Mutura ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia walizikwa jana (Agosti 13) nyumbani kwao katika kijiji cha Kithangari kaunti ya Embu kwenye hafla ilijawa na majonzi.

Picha zilizoonyesha mama ya vijana hao wawili, Catherine Wawira akiwezwa na hisia za majonzi na kuangua kilio kikubwa mbele ya waombolezaji wakati wa mazishi zilivunja nyoyo za Wakenya wengi ambao walishinikiza idara ya upelelezi kufanya hara kupata majibu kuhusiana na tukio hilo.