Mwili wa msichana, 11, aliyekuwa ametoweka Homabay wapatikana umefungwa kwenye mti ukiwa na ishara za kunajisiwa

Mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa umeegemzwa kwenye mti huku shingo yake ikiwa imefungiliwa kwa mti ule kutumia kamba ya mkonge.

Muhtasari

•Inatuhumiwa kuwa Typhan Atieno Odero alinajisiwa kabla ya kuuliwa na kuachwa kichakani.

•Chifu alisema kuwa kulingana na namna mwili wa marehemu ulikuwa umekaa, haiwezekani kuwa alijitoa uhai mwenyewe.

crime scene
crime scene

Habari na Robert Omollo

Msichana wa miaka 11 kutoka kisiwa cha Takawiri, Suba Kaskazini ambaye alitoweka siku  ya Jumapili amepatikana akiwa maiti.

Inatuhumiwa kuwa Typhan Atieno Odero alinajisiwa kabla ya kuuliwa na kuachwa kichakani.

Chifu wa eneo la Mfangano Mashariki, Samwel Dele amesema kuwa wanashuku kuwa wauaji wa msichana huyo walimnajisi kabla ya kumuua kwani kulikuwa na ishara ya damu iliyokuwa inatoka kwenye uke wake.

Alisema kuwa kulingana na namna mwili wa marehemu ulikuwa umekaa, haiwezekani kuwa alijitoa uhai mwenyewe.

Mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa umeegemzwa kwenye mti huku shingo yake ikiwa imefungiliwa kwa mti ule kutumia kamba ya mkonge.

"Tuliitwa katika eneo la tukio na mimi ndiye nilikata kambaambayo ilikuwa imetumika kufunga shingo ya msichana huyo. Kuna damu ilikuwa inatoka kwenye uke wake" Dwele alisema.

Kiongozi huyo alisema kuwa kuna uwezekano marehemu alinajisiwa na mtu wanayefahamiana na akaamua kumuua ili kumnyamazisha na kuficha ushahidi.

Atieno ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya Takawiri  alitoweka alipokuwa anatoka nyumbani kwa wazazi wake katika kisiwa cha Takawiri. Inasemekana kuwa marehemu alikuwa anarejea kwa jamaa wake ambako amekuwa akiishi.

Baada ya kukosa kufika alikokuwa anaenda, familia yake ilianza kumtafuta kwa udi na uvumba na ndipo mwili wake ulipatikana siku ya Jumanne.

Uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kubaini kilichotokea.