Jamaa ahukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kunajisi bintiye wa kambo Nairobi

Mdhulumiwa alisema kuwa alihisi uchungu kwenye sehemu zake za siri na mwanaume yule alikuwa amelala kando yake ila hakujua kilichokuwa kimeingia pale

Muhtasari

•Mwanaume huyo alihukumiwa na hakimu mkuu Philip Mutua baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yake.

•Mdhulumiwa alisema kuwa mwanaume yule alitishia kumuua ikiwa angeambia mtu yeyote na akaendelea kumdhulumu kingono mara kwa mara.

court
court

Habari na Clause Masika

Mahakama ya Kibera imehukumu mwanaume mmoja kifungo cha miaka ishirini gerezani kwa kunajisi binti wake wa kambo miaka mitano iliyopita.

Mwanaume huyo alihukumiwa na hakimu mkuu Philip Mutua baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yake.

Mshtakiwa anasemekanaa kufanya kitendo hicho mwezi Aprili mwaka wa 2016 katika maeneo ya Riruta, Nairobi na kushtakiwa na kosa la kufanyia mtoto kitendo kisichofaa.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 6 ikiwemo daktari na mpelelezi ambao walithibitisha kuwa mshtakiwa alitekeleza kitendo hicho.

Alipokuwa anatoa ushahidi wake, mtoto yule alisema kuwa mama yake alikuwa ameenda nyumbani kwao kijijini na ilibidi amuache na mwanaume huyo aliyemfahamu kama baba yake.

"Nilikuwa nalala kwa sofa ila siku moja nikajipata uchi kitandani cha baba wa kambo" Msichana yule aliambia mahakama.

Mdhulumiwa alisema kuwa alihisi uchungu kwenye sehemu zake za siri na mwanaume yule alikuwa amelala kando yake ila hakujua kilichokuwa kimeingia pale.

Alisema kuwa mwanaume yule alitishia kumuua ikiwa angeambia mtu yeyote na akaendelea kumdhulumu kingono mara kwa mara.

"Siku moja alikuja akanichukua kutoka kwa sofa na akaninajisi sakafuni. Aliniambia kuwa angeniua ikiwa ningeambia mama yangu ama mtu mwingine kuhusu kitendo hicho" Alisema.

Hata hivyo aliarifu rafiki ya mamake kuhusu yale kwani jamaa yule alikuwa na mazoea ya kumpiga kwa rungu mara kwa mara.

Kwa upande wake mshtakiwa alisema kuwa mashtaka dhidi yake yalikuwa uongo wa kutengenezwa tu na kudai kuwa alikuwa na uhusiano mbaya na mama ya mtoto yule. Hata hivyo vipimo vya kidaktari viliashiria kuwa msichana yule alinajisiwa.