Jamaa auwa mwanafunzi wa sekondari kwa upanga baada ya kumfumania akijiburudisha na mkewe kitandani Nakuru

Muhtasari

•Mwanafunzi huyo wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Kapsumbeiywo, kaunti ya Nakuru alidungwa mara kadhaa mwilini kwa upanga mkali hadi na kuachwa akiwa hali mahututi.

Image: HISANI

Ama kweli mke wa wenyewe sumu!

Kijana mmoja mwanafunzi wa shule ya upili alipoteza maisha yake siku ya Jumatatu wakati jamaa mwenye ghadhabu alirejea nyumbani kwake na kumfumania akijiburudisha na mkewe kitandani.

Edmond Kipngetich (19) ambaye alikuwa mwanafunzi wa  kidato cha nne katika shule ya upili ya Kapsumbeiywo, kaunti ya Nakuru alidungwa mara kadhaa mwilini kwa upanga mkali hadi na kuachwa akiwa hali mahututi.

Nduru za mhasiriwa ziliita majirani ila juhudi zao za kumuokoa ziliangulia patupu.

Japheth Bii ambaye alienda mafichoni punde  baada ya kutekeleza kitendo hicho alipandwa na hasira tele na kuchukua upanga alipopata kijana yule kitandani chake wakiwa na mkewe mwenye umri wa miaka 35.

Kulingana na ripoti ya polisi kijana yule alipoteza maisha yake wakati alikuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Nakuru Level 5 kulingana na majeraha mabaya aliyoangamia mwilini.

Polisi wameanza juhudi za kumtafuta Bii.