Ruto alitaka kudhoofisha serikali ya Uhuru, asema Tuju

Muhtasari

• Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju ameibua madai mapya kwamba naibu rais William Ruto si kiongozi bora wa kumrithi rais Kenyatta kwa sababu alitaka kuhujumu serikali ya Jubilee.

• Katibu huyo wa chama cha Jubilee alisema kwamba naibu rais alikuwa na njama ya kuhujumu uongozi wa rais Kenyatta na kuzua mtafaruku ndani ya serikali.

Katibu mkuu wqa chama cha Jubilee
Image: EZEKIEL AMING'A

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju ameibua madai mapya kwamba naibu rais William Ruto si kiongozi bora wa kumrithi rais Kenyatta kwa sababu alitaka kuhujumu serikali ya Jubilee.

Tuju alisema haya Ijumaa - Februari 4, siku ambayo rais Kenyatta alitarajiwa kukutana na wajumbe wanaoegemea mrengo wa Jubilee katika ikulu ya Nairobi.

Tuju amesema kwamba tabia za naibu rais si za kuaminika na kuwataka wakenya wasicheze karata na mustakabali wa maisha yao kwa kumchagua Ruto kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tabia ni muhimu sana, lazima muangalie tabia ya mtu kabla ya kumchagua,” Tuju alisema.

Katibu huyo wa chama cha Jubilee alisema kwamba naibu rais alikuwa na njama ya kuhujumu uongozi wa rais Kenyatta na kuzua mtafaruku ndani ya serikali.

Amesema kwamba katika mbinu ya kufanikisha hujuma hii, Ruto alimfuata kinara wa ODM Raila Odinga mapema kabla ya makubaliano ya Handshake ya mwaka 2018 na kumtaka waungane ili kumuondoa rais Kenyatta madarakani.

Uhuruto
Uhuruto

“Ruto alikuwa wa kwanza kumfuata Raila na kumtaka wageuze serikali ya rais Kenyatta,” Tuju alisema.

Kulingana na Waziri huyo asiye na wizara maalum, rais Kenyatta alisikia uvumi huu na kutibua njama hiyo kwa kumfuata Raila kabla ya naibu wake kufanya hivyo.

Tuju ameyaibua madai haya yenye uzito katika mahojiano katika runinga ya Inooro, asubuhi ya Februari 4.

Katibu huyo amesema pia kwamba naibu rais amekuwa akihangaika usiku na mchana ili kujaribu kudhoofisha chama tawala cha Jubilee baada ya kupoteza uungwaji mkono chamani humo.

Mwezi Januari, naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe pia aliyaibua madai kama hayo kwa kusema kwamba rais Kenyatta alikatiza urafiki wake wa kisiasa na naibu rais alipogundua kwamba Ruto ana njama ya kuhujumu uongozi wake.

Akizungumza katika uga wa Thika, Murathe alisema kwamba naibu rais alikuwa amepewa karibu nusu ya uongozi wa serikali ya Jubilee zikiwemo wizara zenye ushawishi mkubwa lakini rais Kenyatta hakuridhishwa na jinsi wizara hizo zilivyokuwa zikiendeshwa.

Msemaje wa naibu, rais Emmanuel Talam katika mahojiano ya kipekee na gazette la The Star amepuuzilia mbali madai hayo na kushangaa ni kwa nini wanaoegemea mrengo wa Handshake wanaibua wakati huu na si kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.