Kenya namba 3 ulimwenguni kwa visa vya mimba za utotoni, 61% ya visa vipya vya HIV ni vijana wa miaka 15-29

Takwimu hizo zinaonesha kuwa visa vya mimba za utotoni na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi vimeongezeka mara dufu tangu 2021.

Muhtasari

• Mwaka wa 2021, Dagoretti kaskazini iliongoza Nairobi katika maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

• Vijana 98 wenye umri wa miaka 10-19 waliambukizwa Ukimwi kila wiki katika mwaka wa 2021.

Katibu wa kudumu katika wizara ya Afya Susan Mochache akitoa takwimu za afya
Katibu wa kudumu katika wizara ya Afya Susan Mochache akitoa takwimu za afya
Image: Susan Mochache (Twitter)

Nchi ya Kenya imeingia katika rekodi za kuichafulia sura kabisa kote ulimwenguni baada ya takwimu mpya za wizara ya afya kusema kwamba Kenya sasa ni ya tatu kote ulimwenguni kwa visa vya mimba za utotoni.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na katibu wa kudumu katika wizara hiyo Susan Mochache, takwimu zinaonesha kwamba nchini Kenya msichana mmoja kati ya wasichana watano waliobaleghe wenye kati ya miaka 15-19 tayari ni mama au ana ujauzito wa mtoto wake wa kwanza.

Takwimu hizo pia hazikusaza visa vya dhuluma za kijinsia na maambukizi ya virusi vya ukwimu ambapo serikali imesema vyote hivyo vitatu ni kama janga la kitaifa linalofaa kupigwa vita na kila mtu.

Kulingana na ripoti hiyo, visa vya maambukizi ya ukimwi miongoni wa vijana waliobaleghe pia vimeongezeka pakubwa ambapo katika mwaka wa 2021 pekee, vijana 98 wenye umri wa miaka kati ya 10-19 waliambukizwa virusi vya ukimwi kila wiki.

“Asilimia 20 ya ripoti za mimba ambazo zipo nchini Kenya ni za wasichana wadogo, na hawqa ni wasichana wenye umri kati ya 10 na 19, na hii ndio maana ripoti kama hii ni suala la kuzungumziwa kitaifa,” Katibu wa kudumu katika wizara hiyo Susan Mochache alisema.

Itakumbukwa pia kwamba mwaka wa 2017 pekee taifa la Kenya lilirekodi visa 67,000 vya mimba za watoto kutoka kwa idadi ya mimba 317,000 zilizoripotiwa kote nchini.

Takwimu hizo zinazama kwa ndani na kuhoji kwamba vijana kati ya umri wa miaka 15-29 wanachangia asilimia 61 ya visa vipya vya maambukizi ya ukimwi.

Katika mwaka uliopita, eneo bunge la Dagoretti ya Kaskazini pekee lilichangia 15% ya visa vipya vya maambukizi ya ukimwi ambao ni zaidi ya vijana 430 wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19 katika kaunti ya Nairobi pekee.