Naibu wa Rais aomboleza kifo cha Mukami Kimathi.

Rigathi alisema kuwa serikali itamteua afisa mkuu atakayesimamia shughuli za mazishi za shujaa huyo

Muhtasari

•Mukami alikuwa miongoni mwa wapigania uhuru wa Mau Mau waliozuiliwa katika gereza la Kamiti Maximum wakati wa harakati za kupigania uhuru.

 


Naibu wa rais Rigathi amuomboleza Mukami kama shujaa aliyesaidia taifa kupata uhuru.
Naibu wa rais Rigathi amuomboleza Mukami kama shujaa aliyesaidia taifa kupata uhuru.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alikuwa miongoni mwa viongozi walioomboleza kifo cha shujaa wa Uhuru Mukami Kimathi ambaye alikuwa mjane wa shujaa wa Mau Mau Dedan Kimathi.

Akizungumza katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee, ambapo alikuwa ameenda kufariji familia kufuatia kifo chake, Gachagua alisema Mukami alikuwa msukumo kwa uongozi wa nchi.

"Kama taifa, tumehuzunishwa sana na kifo chake. Alikuwa kielelezo cha matumaini sio tu katika eneo la Kati lakini nchi nzima," Rigathi alisema.

Gachagua alisema kuwa serikali itamteua afisa mmoja mkuu atakayesimamia shughuli za mazishi ya Mukami.

"Afisa huyu mkuu atashirikiana na familia kumpa Mukami mazishi inayomfaa," Rigathi aliongeza.

Naibu Rais pia alisikitika kwamba mashujaa wa uhuru wamekuwa wakiishi katika hali ya uchochole licha ya kuchangia uwepo wa taufa la Kenya.  

"Haya ni maswala tutakayojadili. Tunapaswa kuangalia jinsi dhuluma za kihistoria zinapaswa kushughulikiwa," alisema Rigathi.

Mukami Kimathi aliyezaliwa mwaka wa 1927  alifariki akiwa na umri wa miaka 96 alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Kulingana na bintiye Evelyn Kimathi shujaa huyo aliagaa dunia Alahamisi usiku.

Mukami alikuwa miongoni mwa wapigania uhuru wa Mau Mau waliozuiliwa katika gereza la Kamiti Maximum wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Alisaidia sana Kenya kupata uhuru wake kutoka kwa wakoloni pamoja na bwana yake Dedan Kimathi.

 Hivi majuzi Mukami alipokea usaidizi wa kifedha kutoka kwa utawala wa Rais William Ruto, ambao ulimsaidia kufuta bili ya hospitali ya Sh1.3 milioni