"Wasiwasi wa nini, pumua kawaida tu!" Junet anamwambia Linturi wakati wa kuhakikiwa bungeni

Linturi alikanusha kuwa ana wasiwasi na kusema hawezi kuwaogopa wabunge hao kwani amefanya kazi na baadhi yao kwa muda mrefu.

Muhtasari

• Linturi amabye ni waziri mteule katika wizara ya kilimo alifika mbele ya kamati ya bunge ya uhakiki Ijumaa asubuhi.

• Alipata wakati mgumu kujibu baadhi ya maswali jambo ambali lilimfanya Junet kuhisi ameingiwa na woga.

Junet amwambia Linturi kuacha woga
Junet amwambia Linturi kuacha woga
Image: Maktaba

Huku mchakato wa kuhakiki na kuwahoji mawaziri wateule katika baraza la mawaziri la rais Ruto ukiendelea kwa wiki moja sasa, Ijumaa ilikuwa zamu ya waziri mteule katika wizara ya kilimo, Mithika Linturi.

Akikabiliwa na maswali makali kutoka kwa kamati ya bunge inayosimamia shughuli hiyo ya kuwahakiki, Linturi alipata wakati mgumu kuelezea baadhi ya skendo zinazolizunguka jina lake pamoja pia na idadi kubwa ya kesi ambazo amekuwa akihusika.

Wabunge walimtia katika kikaango mpaka mmoja wao – mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed kuhisi kwamba Linturi alikuwa ameingiwa na wasiwasi na hata pumzi  zake kupanda kwa kasi isiyo ya kawaida.

Hivyo, Junet aliomba spika Wetang’ula nafasi na kutoa ombi lake akimtaka spika kumwambia Linturi kukoma kupumua kwa kasi kama mtu ambaye ameingiwa na wasiwasi.

“Mwambie apumue kawaida, anaonekana kuwa na wasi wasi, anapumua kwa kasi sana,” Junet alisema huku akiiga vishindo vya kupumua akiambatanisha na kicheko kikubwa kabla ya wabunge wenzake kuangua kicheko pia.

Suala hilo ambalo lilionekana kama utani lilimfanya spika ambaye kinadharia ndiye mwenyekiti wa kamati huyo kumuuliza Linturi kama ni kweli alikuwa na woga na wasi wasi kuwekwa kwenye kiti moto na wabunge hao.

Linturi ambaye alikuwa mbunge wa Igembe South kabla pia ya kuwakilisha kaunti ya Meru katika bunge la seneti alikana madai hayo ya Junet na kusema kwamba hana wasiwasi wowote.

“Hapana, sina wasiwasi. Ninawezaje kuwa na woga na hawa ndio watu ambao tumefanya kazi nao kwa muda mrefu?” Linturi alijibu huku akijitetea dhidi ya kuonesha woga.