Sidika, Anerlisa wafariji Davido kufuatia kifo cha mwanawe, wamuombea kupata mapacha

Mtoto wa Davido aliaga dunia mapema wiki hii baada ya kudaiwa kuzama katika bwawa la kuogelea la nyumbani.

Muhtasari

• Naomba Mungu awafariji, awape Amani na utulivu pamoja na ujasiri wa kukabiliana na kipindi hiki kigumu - Vera Sidika aliandika.

Vera na Anerlisa wamufariji Davido
Vera na Anerlisa wamufariji Davido
Image: Instagram

Vera Sidika na Anerlisa Muigai wameungana na familia ya mwanamuziki kutoka Nigeria Davido kumuomboleza mwanao aliyeaga dunia mapema wiki hii kwa kuzama katika bwawa la kuogelewa la nyumbani.

Taarifa hizo za tanzia zilisagaa mitandaoni huku baadhi wakihisi ni porojo kwani mpaka sasa msanii Davido hajasema lolote lililotokea wala kuzungumzia mazingira ambayo yalisababisha mwanawe kufa maji.

Kupitia kurasa zao za Instagram, mwanasosholaiti Vera Sidika na mrithi wa kampuni ya Keroche Anerlisa Muigai walimpa shavu Davido na kusema walikuwa wanahisi kile ambacho yeye na mkewe Chioma walikuwa wanapitia wakati huu wa majonzi.

Sidika alisema kwamba yeye kama mzazi anajua fika uchungu wa kumpoteza mtoto kamwe hauwezi ukatulizwa wala kuondolewa kwa maneno yoyote hata yawe matamu vipi lakini akamfariji Davido kwa njia ya kipekee huku akiwaombea Mungu kuwapa faraja.

“Leo imekuwa siku mbaya sana, habari za kuvunja moyo sana kama mama siwezi nikajivika viatu vya Chioma na Davido. Naomba Mungu awafariji, awape Amani na utulivu pamoja na ujasiri wa kukabiliana na kipindi hiki kigumu,” Vera Sidika aliandika.

Kwa upande wake, Anerlisa Muigai alishauri watu kwamba katika dunia ya sasa iliyojawa na watu wenye roho nyeusi, ni lazima uwe na tahadhari kubwa kuhusu watu wanaokuzunguka na kuzunguka watoto wako.

Aliwaombea Davido na mkewe kupata faraja ya kipekee itokayo kwa Mungu.

“Katika dunia hii ambayo imejaa watu wenye husda pamoja na ajali nyingi, ni sharti tuwe waangalifu kwa kupitilizia katika watu ambao wanatuzunguka. Nawaombea kupona na kupata faraja na pia kuwaombea Mungu kuwajaalia mapacha wa kuziba pengo ambalo limeachwa na marehemu mwanao,” Arnelisa Muigai alisema.