Familia ya Kenyatta imesema tuiache peke yao! - Waziri wa Ulinzi Aden Duale

"Ndio familia tajiri zaidi barani Afrika na wametuma wajumbe kwamba Rais wa zamani na familia yake waachwe peke yao,"

Muhtasari

• Shamba la Kenyatta lilishambuliwa na kuibua madai kwamba ulinzi wa familia hiyo ya kwanza ulipunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Mbunge wa Garissa Aden Duale
Mbunge wa Garissa Aden Duale
Image: MAKTABA

Waziri wa ulinzi Aden Duale ameibua madai mapya kwamba familia ya Kenyatta imetuma wajumbe kwa serikali ikitaka kuachwa peke yao bila kupewa ulinzi.

Jina la Uhuru limekuwa kwenye vichwa vya habari wiki za hivi karibuni baada ya baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kumshutumu Rais huyo wa zamani kwa kufadhili maandamano ya kupinga serikali yanayoendelea yakiongozwa na kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, shutuma ambazo rais huyo wa zamani amekanusha vikali.

Shamba linalomilikiwa na familia ya Kenyatta la Northlands huko Ruiru pia lilivamiwa na waandamanaji siku ya Jumatatu na kipande chake kiliharibiwa wakati wa maandamano hayo, na kumweka Mkuu wa zamani wa Nchi na familia yake kwenye gumzo la vyombo vya habari tena.

Katika uvamizi huo, idadi ya kondoo isiyojulikana aina ya Dorper waliripotiwa kuibwa na watu hao ambao baadhi walikuwa na njama ya kugawanya shamba hilo, na wengine hadi kujenga kambi za mabati katika shamba hilo kabla ya kuchoma sehemu ya shamba hilo.

Hata hivyo, siku mbili baadae, iliharifiwa kwamba maafisa wa kutoa ulinzi kadhaa walionekana katika shamba hilo na kuanza kuweka ulinzi huku wengine kadhaa pia wakionekana katika boma la Kenyatta nyumbani kwake, Ichaweri, kaunti ya Kiambu.

Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio mnamo Ijumaa, CS Duale alidai kuwa Uhuru na jamaa zake sasa wanataka kuachwa nje ya umaarufu baada ya wiki kadhaa za kuangaziwa.

"Ndio familia tajiri zaidi barani Afrika na wametuma wajumbe kwamba Rais wa zamani na familia yake waachwe peke yao," alisema Duale.

Hata hivyo, Duale alisema kwamba serikali haijatathmini kama itaacha familia hiyo peke yao kama walivyodai kwani huenda wakahitaji kuifanyia uchunguzi wa jinsi Kenyatta alitumia fedha za umma kipindi anaongoza Kenya.

Duale vile vile alimshutumu Bw Odinga kwa kuchochea maandamano dhidi ya serikali kwa vile anadaiwa anataka tu kuwa sehemu ya serikali ya Kenya Kwanza, lakini kupitia mlango wa pembeni.