Ruto asusia mkutano wa kuzindua ripoti ya BBI

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto

Naibu rais William Ruto alikosa kuhudhuria hafla ya Jumatano ya uzinduzi wa ripoti ya BBI ilipokuwa inakabidhiwa rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Badala yake, Ruto alihudhuria mazishi ya Mwakilishi wadi wa Huruma Peter Chomba, aliyefariki kutokana na maradhi ya Covid-19.

Baada ya kuhudhuria maadhimisho ya siku kuu ya Mashujaa katika kaunti ya Kisii siku ya Jumanne, Ruto alisafiri hadi nyumbani kwake katika kaunti ya Uasin Gishu ili kuhudhuria mazishi ya Chomba. 

Kaka mkubwa wa marehemu Lenny Chomba na mjomba wake Kiiru Chomba walisema kwamba upasuaji wa mwili wa mwenda zake ulibaini kwamba alifariki kutokana na matatizo ya virusi vya covid-19.

Ruto katika hotuba yake fupi siku ya Mashujaa alitoa wito kwa rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kuhusisha wakenya wote kwenye mchakato wa BBI.

Ruto alisisitiza umuhimu wa kujumuisha kila mtu ili kuafikia azimio la kuunganisha taifa. 

Naibu rais alitaka pawepo mjadala wa kitaifa unaohusisha maoni ya kila mkenya katika mchakato wa BBI. 

Ruto amekuwa mkosoaji mkuu wa BBI, huku akitaja zoezi hilo kama la kutafutia watu wachache nyadhifa badala ya kuangazia matakwa na wananchi wa kawaida.