Serikali haitakulelea mtoto, wazazi waonywa

Muhtasari

• Wazazi watakiwa kuajibikia malezi ya watoto wao.

• Kiwango cha uwajibikaji wa wazazi ni cha chini mno.

• Watoto 44 walinaswa wakinywa pombe katika nyumba ya kibinafsi.

Bidhaa zilizonaswa katika nyumba walimokuwa watoto wakisherehekea. Picha Mercy Mumo
Bidhaa zilizonaswa katika nyumba walimokuwa watoto wakisherehekea. Picha Mercy Mumo

Wazazi  wametakiwa kuajibikia malezi ya wanao hasa wakati huu ambapo watoto wengi wako nyumbani baada ya shule kufungwa kutokana na janga la Korona.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Martiang’i alisema ni jambo la kusikitisha kuona watoto wadogo wakishikwa wakijihusisha na mambo yasiofaa.

Alitoa tahadhari kuhusu kupotoshwa kwa vijana na watu wenye hila na wenye nia mbaya.

"Kiwango cha uwajibikaji wa wazazi ni cha chini mno …Jamii na serikali hazitalea watoto wako," alisema.

Waziri alitowa wito kwa wazazi kuwajibikia malezi ya wanao ili kuzuia matukio ya hivi punde ambapo watoto wengi wamekamatwa na maafisa wa usalama wakijihusisha na ulevi, matumizi ya mihadarati na hata kushiriki ngono.

Mwishoni  mwa wiki maafisa wa polisi baada ya kudokezewa waliwanasa takriban watoto 44 katika nyumba moja mtaani Mountain View mjini Nairobi wakishiriki ulevi, mihadarati mingine na maovu mengine mengi. 

Chupa kadhaa za vileo na kondomu zilizokuwa zimetumika zilinaswa katika eneo hilo.

Watoto walionaswa walikuwa wa kati ya umri wa miaka 14-17 na inasemekana wote ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Mama mwenye nyumba walimokuwa ‘amezuiliwa kwa siku saba huku uchunguzi ukiendelea.

Wanafunzi wamekuwa nyumbani tangu mwezi Machi baada shule kufungwa kutokana na janga la korona. Tayari wizara ya elimu imetangaza kwamba shule zote zsutafunguliwa tarehe 4, Januari mwakani.