Mauaji ya wakili Syokimau, polisi wamsaka raia wa Nigeria

Uhalifu
Uhalifu

Maafisa wa upelelezi wanamsaka raia wa kigeni ambaye anashukiwa kwa mauaji ya wakili mashuhuri mwanamke ambaye alikuwa akiishi naye huko Syokimau, Kaunti ya Machakos.

Wapelelezi walisema Ijumaa jioni kwamba kwa mujibu wa ripoti yao, mshukiwa ambaye ana pasipoti ya Nigeria alionekana akitoka nyumbani kwa mwathiriwa Alhamisi usiku. Mwili wa wakili huyo mashuhuri ulipatikana chumbani mwake Ijumaa asubuhi.

Kulingana na polisi, tukio hilo lilithibitishwa na mfanyikazi wa nyumba ywa wakili huyo, ambaye alishuku kitu baada ya mwajiri wake kutokuwa ameamka saa nne asubuhi.

 

Alipoingia chumbani mwake alishtuka kumuona akiwa amelala bila uhai kitandani, huku mwili wake ukiwa na damu.

Polisi bado wanashughulikia eneo la uhalifu huku wapelelezi wakiimarisha msako dhidi ya mshukiwa anayejulikana kama Christian Kadima Mwambay.

Wananchi wametakiwa kuripoti habari ambazo zitasaidia polisi kumkamata mshukiwa. Habari inaweza kuripotiwa kupitia nambari ya biila malipo ya DCI 0800 722 203.