Maraga astaafu rasmi kutoka idara ya mahakama

Muhtasari

•  Alimkabidhi mamlaka naibu jaji mkuu Philomena Mwilu ambaye atahudumu kama kaimu Jaji Mkuu hadi pale jaji mkuu mwingine atakapoteuliwa.

  • Alichukuwa hatamu kuongoza idara ya mahakama mwaka 2016 baada ya kustaafu kwa Willy Mutunga.   

Jaji mustaafu David Maraiga aondoka makao makuu ya Mahakama ya juu akiwa mwananchi wa kawaida baada kustaafu rasmi.
Jaji mustaafu David Maraiga aondoka makao makuu ya Mahakama ya juu akiwa mwananchi wa kawaida baada kustaafu rasmi.

David Kenani Maraga amestaafu rasmi kutoka wadhifa wa jaji mkuu na rais wa mahakama ya juu baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne.

Maraga siku ya Jumatatu alimkabidhi mamlaka naibu jaji mkuu Philomena Mwilu ambaye atahudumu kama kaimu Jaji Mkuu hadi pale jaji mkuu mwingine atakapoteuliwa.

Jukumu la mwisho la Maraga lilikuwa siku ya Jumatatu asubuhi alipoongoza kikao cha mahakama ya juu kilichoandaliwa kwa heshima yake.

 

Hafla ya kustaafu kwake ilihudhuriwa na familia yake, viongozi wa makanisa, mawakili na majaji.

Katika hafla hiyo ya kufana nje ya makao makuu ya mahakama ya juu Maraga alivuliwa nguo zake rasmi za kazi na gari lake likaondolewa nambari rasmi za Jaji mkuu ‘CJ 1’ na bidhaa  hizo zote zilikakabidhiwa msajili mkuu wa mahakama Anne Amadi.

David Maraga akivuliwa magwanda ya kazi baada ya kustaafu
David Maraga akivuliwa magwanda ya kazi baada ya kustaafu

Maraga ambaye amehudumu katika idara ya mahakama kwa kipindi cha miaka 18 aliondoka katika gari lake la kibinaffsi akiandamana na familia yake akiwa raia wa kawaida.

Katika hotuba yake ya mwisho Maraga alitoa wito kwa maafisa wa idara ya  mahakama kutekeleza majukumu yao kwa ujasiri bila uoga na mapendeleo.

Aliwataka kuzingatia sheria na katiba ya taifa na kumuomba Mungu kwa kila jambo.

Jaji huyo mustaafu alikiri kwamba safari yake kama Jaji mkuu haikuwa raihisi na kwamba alipokea vitisho chungu nzima kutokana na kazi yake.

 “Nataka kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa nafasi hii kuhudumia watu wa Kenya na muongozo aliyonipa,” alisema.

Kaimu jaji mkuu Philomena Mwilu baada ya kukabidhiwa mamlaka na David Maraga.
Kaimu jaji mkuu Philomena Mwilu baada ya kukabidhiwa mamlaka na David Maraga.
 

Maraga aliwakumbusha wakenya vile alichagua imani yake dhidi ya kazi ya Jaji mkuu.

Aliwashukuru wakenya kwa jumla kwa kusimama naye kila mara na kumuunga mkono.

"Mshikamano wenu na ulinzi thabiti wakati wa majaribio viliimarisha azimio langu la kuwatumikia hadi leo," alisema.

Maraga atakumbukwa kwa kuongoza kikao cha mahakama ya juu kilichofutilia mbali uchaguzi wa urais mwaka 2017.

Alichukuwa hatamu kuongoza idara ya mahakama mwaka 2016 baada ya kustaafu kwa Willy Mutunga.