Afueni huku chanjo ya covid-19 ikitua Kenya

Muhtasari

• Chanjo hiyo ya AstraZeneca iliagizwa kutoka taasisi ya Serum ya India.

• Takriban watu milioni 1.25 wanatarajiwa kupokea njacho hiyo nchini Kenya katika awamu ya kwanza.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe (wa pili kulia) akiongoza maafisa wengine kupokea chanjo ya COVID-19 katika uwanja wa JKIA
Waziri wa afya Mutahi Kagwe (wa pili kulia) akiongoza maafisa wengine kupokea chanjo ya COVID-19 katika uwanja wa JKIA

Hayawi hayawi huwa, hatimaye chanjo ya Covid-19 ishatua nchini Kenya.

Shehena ya kwanza ya takriban chanjo milioni moja ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa JKIA usiku wa kuamkia Jumatano na kupokelewa na waziri wa Afya Mutahi Kagwe miongoni mwa viongozi wengine wakuu katika serikali.

"Kwa kweli ni siku njema kwa Kenya. Sasa tuna silaha sawa na bazooka au machine gun katika vita vyetu dhidi ya virusi, "Waziri Kagwe alisema punde tu shehena ya chanjo ya covid-19 ilipotua uwanja wa JKIA.

Chanjo hiyo ya AstraZeneca iliagizwa kutoka taasisi ya Serum ya India.

Serikali ilitangaza kwamba wahudumu wa afya watakuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo ili kupata kikinga ya kutosha dhidi ya virusi hivyo wanapo wahudumia wakenya.

Watu wengine wanaotarajiwa kuwa katika makundi ya kwanza kupokea chanjo hiyo ni walimu, maafisa wa usalama wahudumu wa mahoteli na watu wenye afya duni miongoni mwa makundi mengine yaliyo katika hatari ya kuambukizwa virusi kulingana na kazi zao.

Katibu mkuu wa chama cha kutetea maslahi ya wanahabari nchini (KUJ) Eric Oduor vile vile ametoa wito kwa serikali kuzingatia wanahabari katika awamu ya kwanza ya chanjo akisema kwamba pia wao wako kwenye mstari wa mbele katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Takriban watu milioni 1.25 wanatarajiwa kupokea njacho hiyo nchini Kenya katika awamu ya kwanza.