Mjadala kuwa Uhuru anamcheza Raila ni wa kusambaratisha BBI

Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya
Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya

Taarifa ya Moses Odhiambo

Kiongozi wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya amepuuzilia mbali madai ya njama ya kumruka kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mbunge huyo wa Kipipiri alisema madai hayo yanasukumwa na watu "wasiofurahishwa na uungwaji mkubwa ambao BBI ilipata katika mabunge ya kaunti."

Angalau mabunge 43 ya kaunti yalipiga kura kupitisha Muswada wa marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2020. Ni mabunge matatu tu - Nandi, Elgeyo Marakwet, na Baringo waliukataa muswada huo.

 

Kimunya aliiambia The Star kwamba mtindo wa upigaji kura kuunga mkono BBI umesababisha mchecheto miongoni mwa watu ambao wameogopa wakati nchi inaelekea kwenye kura ya maoni.

Washirika wa Raila mwishoni mwa wiki walimpa rais Uhuru makataa kumwondoa Katibu wa kudumu wa Mambo ya Ndani Karanja Kibicho kutoka kwa mipango ya kupigia debe BBI, na kufichua kuwepo kwa malumbano katika kambi ya handshake.

Kiranja wa Wachache Junet Mohamed, Seneta wa Siaya James Orengo, na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo - ambao ni wandani wa Raila – waliibua mjadala mkali na kufichua uhasama ambao ulikuwa unakita mizizi katika handshake.

Walizungumza kuhusu njama ya watu mashuhuri katika Ofisi ya Rais kumtenga Raila kwa kupendelea kambi inayowaleta pamoja kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Seneta wa Baringo Gideon Moi (Kanu), na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Lakini Kimunya alisema madai kuwa Raila au washirika wake wametengwa ni "hila y watu ambao wamepoteza sana ushawishi kutokana na mabunge ya kaunti kupitisha BBI."

"Kuna watu ambao walishtuka, ambao walidhani BBI haendi popote. Sasa wanasongwa na mawazo na kuambia ODM mambo ya kuwakera. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu ndani ya ODM huenda waliingia mtegoni, "Kimunya alisema.

Alisema juhudi za wapinzani - ambao anasema ni washirika wa kikundi cha Tangatanga - ni kusambaratisha BBI isipate umaarufu kwenda mbele.

Kimunya aliondoa hofu akisema kwamba "Rais Uhuru Kenyatta na kaka yake Waziri Mkuu wamejitolea sana kwa mchakato wa BBI."