Naibu gavana wa Nairobi atangaza kugombea ugavana 2022

Muhtasari

• Licha ya kesi za mahakamani zinazoendelea kuhusu wadhifa wake, kazi katika serikali ya kaunti ya Nairobi imekuwa ikiendelea bila tatizo.

• Tangu aingie ofisini, Kananu amefanya kazi kwa karibu na baraza lake la mawaziri na wafanyikazi wa kaunti kuhakikisha kuwa huduma zinaendelea.

Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Anne Kananu akiapishwa naibu gavana wa Nairobi, Januari 15, 2021.
Image: EZEKIEL AMINGA

Taarifa ya Maureen Kinyanjui 

 

Takriban miezi mitatu ofisini, Naibu Gavana wa kaunti ya Nairobi Anne Kananu ameonyesha uongozi wa mabadiliko ambao umeleta utulivu katika Jumba la City Hall.

 

Licha ya kesi za mahakamani zinazoendelea kuhusu wadhifa wake, kazi katika serikali ya kaunti ya Nairobi imekuwa ikiendelea bila tatizo.

Mwishoni mwa wiki, Kananu alitangaza kuwa atawania ugavana wa Nairobi mwaka ujao.

 

Tangazo lake linaweza kuwa la kushangaza, lakini wale walio karibu naye lazima waliliona likija.

Hata hivyo labla kilichowashangaza ni wakati wa kutolewa kwa tangazo hilo.

Alipochukua madaraka kutoka kwa spika wa bunge la kaunti Benson Mutura, ambaye alikuwa kaimu gavana, Kananu alisema lengo lake lilikuwa kuleta uongozi mpya katika kaunti.

"Mimi sio mwanasiasa, na sitaanza kuwa mmoja. Ninalenga kuleta muamko mpya wa ushirikiano, mshikamano na kuheshimiana na vyombo vyote vya serikali. Nairobi sasa imerejea," alisema.

Hata hivyo, baada ya kutangaza nia yake kuania kiti cha gavana, aliwaonya wapinzani kujipanga kwa densi ngumu ya kisiasa katika mji mkuu wa Kenya.

 

"Nitashindana katika uchaguzi wa 2022. Kwa wale ambao wanafikiria niko hapa kwa muda kidogo, ninawaambia kuwa niko hapa kukaa. Tutapambana," Kananu alisema.

Kuinuka kwake kisiasa kumechukua muda mfupi na imekuwa bahati kuwa naibu gavana wa kwanza mwanamke wa Nairobi.

 

Kabla ya Januari 15, 2021, Kananu alikuwa amehudumu kama katibu wa kushughulikia majanga kwa miaka mitatu.

Alikuwa ameolewa kwa Philip Njiru Muthathai, ambaye alifariki Januari 2019, kutokana na ajali ya barabarani.

Aliyekuwa Gavana Mike Sonko alimteua kuwa naibu gavana Januari 6, 2020, lakini mahakama ilizuia bunge la kaunti kumpiga msasa.

Baada ya mahakama kuondoa kesi hiyo, Kananu aliapishwa kama naibu gavana wa Nairobi hatua ambayo ilizuia kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ugavana kufuatia kuondolewa kwa Mike Sonko.

Kugombea kwake kutazamwa kama msukumo kwa wanawake na vijana wanaotamani kuwa viongozi nchini.

Tangu aingie ofisini, Kananu amefanya kazi kwa karibu na baraza lake la mawaziri na wafanyikazi wa kaunti kuhakikisha kuwa huduma zinaendelea.

Ameongoza baraza lake la mawaziri katika mikutano, akisaidiwa na kaimu katibu wa kaunti Jairus Musumba.