Mwalimu mkuu akamatwa kwa madai ya wizi wa mtihani - Machakos

Muhtasari

• Betta Mutuku mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya ABC Kiseveni katika kaunti ndogo ya Machakos alikamatwa na maafisa wa DCI Jumanne asubuhi.

• Simu ya mwalimu huyo mkuu ilichukuliwa na maafisa wa polisi kusaidia katika uchunguzi.

Afisa mkuu wa DCI Machakos Rhoda Kanyi (kushoto) akiandamana na mwalimu mkuu wa shule ya ABC Kiseveni Betta Mutuku Aprili 6, 2021.
Afisa mkuu wa DCI Machakos Rhoda Kanyi (kushoto) akiandamana na mwalimu mkuu wa shule ya ABC Kiseveni Betta Mutuku Aprili 6, 2021.
Image: GEORGE OWITI

Mwalimu mkuu wa shule moja katika kaunti ya Machakos amekamatwa kwa madai ya wizi wa mtihani ya KCSE.

Betta Mutuku mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya ABC Kiseveni katika kaunti ndogo ya Machakos alikamatwa na maafisa wa DCI Jumanne asubuhi.

Wapelelezi waliongozwa na Afisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Machakos Rhoda Kanyi ambaye alisema waliafuatilia taarifa za kijasusi kumkamata mwalimu huyo.

Kanyi alisema mwalimu huyo anashukiwa kuchukua picha ya karatasi ya mtihani wa KCSE wa leo na kuipakia kwenye ukurusa wake wa WhatsApp kwa watahiniwa kusoma.

Hata hivyo alisema kwamba mwalimu huyo alisema kwamba si yeye aliweka karatasi hilo kwa simu yake. Karatasi hilo liliwekwa Jumatatu jioni.

Mshukiwa alipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Machakos ambapo anahojiwa na maafisa wa CID.

"Alikuwa ameweka mitihani kwa ukurasa wake ili watahiniwa wasome usiku," Kanyi aliwaambia waandishi wa habari.

Simu ya mwalimu huyo mkuu ilichukuliwa na maafisa wa polisi kusaidia katika uchunguzi.

Tukio hilo lilitokea karibu wiki moja tangu watahiniwa watano wakamatwe kwa madai ya kuiba mitihani Alhamisi iliyopita.