Mshukiwa wa mauaji ya afisa wa tume ya ardhi ana akili timamu

Muhtasari

• Alifanyiwa vipimo vya akili na uchunguzi maalum wa kumtambuwa wiki iliyopita.

• Washukiwa wengine wawili katika kesi hiyo -Benjamin Saitoti, mwendeshaji wa boda boda, na David Sempuan, mfugaji - wameachiliwa huru na kuwekwa chini ya ulinzi wa mashahidi.

Marehemu Jennifer Wambua
Marehemu Jennifer Wambua
Image: HISANI

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa zamani wa Tume ya Ardhi Jennifer Wambua yuko sawa kiakili kushtakiwa.

Polisi wanatarajia kueleza mahakama ya Kiambu kuwa Peter Njenga alias Ole Sankale, mwenye umri wa miaka 44 yuko na akili timamu na kwa hivyo atakabiliwa na mashtaka ya mauaji.

Mshukiwa pia anakabiliwa na mashtaka mengine ya uhalifu, pamoja na ubakaji na wizi wa mabavu.

Alifanyiwa vipimo vya akili na uchunguzi maalum wa kumtambuwa wiki iliyopita kabla ya vikao vya leo.

Washukiwa wengine wawili katika kesi hiyo -Benjamin Saitoti, mwendeshaji wa boda boda, na David Sempuan, mfugaji - wameachiliwa huru na kuwekwa chini ya ulinzi wa mashahidi.

Hao ni mashahidi wa upande wa mashtaka dhidi ya Njenga.

 Uchunguzi wa kimaabara uliweka Njenga katika eneo la uhalifu. Uchunguzi huo ulimtambua vyema kama mtu ambaye alikuwa na marehemu kabla ya mwili wake kupatikana.

Wambua alipotea mnamo Machi 12, 2021 kabla ya mwili wake kupatikana katika eneo la Kerarapon, Ngong siku iliyofuata.