Knut imeamka kutoka usingizini - Collins Oyuu

Muhtasari

• Katibu Mkuu wa KNUT Collins Oyuu alisema kuwa Knut imeamka kutoka usingizi mrefu na watatilia maanani mazungumzo bila maandamano barabarani.

• Oyuu alisema wameipa TSC wiki moja kurekebisha mapendekezo yake kabla ya mkutano mwingine na miungano ya walimu.

Katibu mkuu wa Knut Collins Oyuu
Katibu mkuu wa Knut Collins Oyuu
Image: MAKTABA

Chama cha Kitaifa cha kutetea maslahi ya Walimu nchini Kenya (KNUT) kimetangaza kufanya mkutano mwingine na Tume ya kuajiri walimu nchini (TSC) ili kuainisha Makubaliano yao ya Pamoja (CBA).

Katibu Mkuu wa KNUT Collins Oyuu alisema wameipa TSC wiki moja kurekebisha mapendekezo yake kabla ya mkutano mwingine na miungano ya walimu.

Katibu mkuu huyo mpya alibaini kuwa mapendekezo ya awali waliyopewa hayakuwa na faida ya kifedha kwa wanachama wa Muungano huo.

Oyuu alisema kuwa Knut imeamka kutoka usingizi mrefu na watatilia maanani mazungumzo bila maandamano barabarani.

Alitangaza kuwa baada ya mkutano ambao haukuzaa matunda kuhusu CBA, alipata mwaliko kutoka kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia ili kujadili mwelekeo mpya kuhusu mkataba wa pamoja.

"Tulijadili sana juu ya CBA na ninaandika ripoti kuwasilisha kwa kamati simamizi ya Kitaifa siku  Jumanne. Ripoti hiyo itatolewa kwa baraza kuu wakati huo".

Oyuu alisema lazima wapate mwafaka ambao utaleta maelewano na amani baina ya mwajiri na wafanyikazi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kisumu siku ya Alhamisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Oyuu alisema ameazimia kurudisha utukufu na hadhi ya muungano huo siku za nyuma.

Alikuwa akirejea katika eneo la Nyanza kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Knut.

Oyuu alisema kwamba jukumu lake kuu kwa sasa ni kuwarudisha wanachama ambao waliondoka KNUT na kujiunga na vyama vingine vya wafanyikazi.

Alifichua kuwa kwa sasa KNUT ina takriban wanachama 15,000, kutoka zaidi ya wanachama 200,000 hapo mbeleni.

Oyuu alisema matawi ya KNUT yapo kwenye hatari ya kufungwa kutokana na ukosefu wa fedha za kuendesha matawi hayo.

Oyuu alichaguliwa katika wadhifa huo bila kupingwa Jumamosi iliyopita baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa muungano huo kwa kipindi kirefu Wilson Sossion Kujiuzulu.