ODM yajiondoa rasmi kutoka kwa muungano wa NASA

Sifuna alisema kuwa chama hicho kiko kwenye harakati ya kuunda ushirikiano na vyama vingine.

Muhtasari

•Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitoa tangazo hilo siku ya Alhamisi na kudai kuwa wangeandikia msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu uamuzi huo.

•Sifuna alisema kuwa mikutano ya maeneo imepangwa tayari kwa ushirikiano na vyama ambavyo vina maono sawa  na ya ODM.

Kamati ya uendeleshaji wa ODM ikiongozwa na Raila Odinga
Kamati ya uendeleshaji wa ODM ikiongozwa na Raila Odinga
Image: TWITTER//RAILA ODINGA

Chama cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri mkuu Raila Odinga kimejiondoa rasmi kutoka kwa muungano wa NASA.

Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitoa tangazo hilo siku ya Alhamisi na kudai kuwa wangeandikia msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu uamuzi huo.

"Tunasisitiza kuwa NASA imekufa. Ili kuthibitisha hayo, kamati ya uendeleshaji wa chama cha ODM hivi leo imeamua kujiondoa rasmi kutoka muungano wa NASA" Sifuna alitangaza.

Sifuna alisema kuwa chama hicho kiko kwenye harakati ya kuunda ushirikiano na vyama vingine.

"Tunakadiria kuanzisha mpango wa kuunda ushirikiano mpya na kuendeleza majadiliano na washirika wetu wapya," Sifuna alisema.

Alisema kuwa mikutano ya maeneo mepangwa tayari kwa ushirikiano na vyama ambavyo vina maono sawa  na ya ODM.

Alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa ODM John Mbadi, mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, mbunge wa kuteuliwa Dennita Ghati na wengineo.

Hatua hiyo inajiri siku tatu tu baada ya chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kutangaza kujiondoa kwake kutoka kwa muungano huo na kujiunga na muungano wa One Kenya Alliance (OKA).