Machifu na manaibu wao walevi kufutwa kazi

Muhtasari

• Waziri wa usalama wa ndani Fred Matyang’i siku ya Alhamisi alitangaza oparesheni kali ya kukabili matumizi na uuzaji wa pombe haramu na dawa za kulevya kote nchini.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matyang'i
Waziri wa usalama wa ndani Fred Matyang'i
Image: twitter.com/FredMatiangi

Machifu na manaibu wao ambao ni waraibu wa vileo wataachishwa kazi.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matyang’i siku ya Alhamisi alitangaza oparesheni kali ya kukabili matumizi na uuzaji wa pombe haramu na dawa za kulevya kote nchini.

Akihutubia makamishna wa kaunti na waratibu wa kanda Matyang’i alisema itakuwa vigumu kwa afisa yeyote wa serikali ambaye ni mraibu wa pombe kuzuia wananchi wengine kutumia pombe haramu.

Alisema kwamba oparesheni ya mwanzo itakayoendelea kwa siku 30 italenga kuenea kwa pombe za viwango duni na haramu ambazo usambazaji wake huongezeka sana uchaguzi unapokaribia.

"Tuna changamoto kubwa ya unywaji pombe unaochochewa na msimu wa uchaguzi. Watu wengine wanafikiria ni wakati wa kutoa pombe ya bei rahisi kuwezesha kampeni, "alisema.

twitter.com/FredMatiangi
twitter.com/FredMatiangi

Waziri ambaye alikuwa akizungumza katika chuo cha mafunzo ya serikali cha Kenya mtaabi Kabete pia aliwataka wasimamizi wa serikali kuwa mfano wa kuigwa na kuonya wale ambao ni waraibu wa pombe na dawa za kulevya kuwa watafutwa kazi.

“Lazima tuwe wakweli na kukiri kwamba tuna shida kutoka ndani. Ikiwa wewe ni afisa mlevi anayetetemeka katika baraza za umma, utatekelezaje msako dhidi ya uraibu wa vileo haramu? Unawezaje kutekeleza sheria wakati unafaa kuwa katika kituo cha kukabili uraibu? ” Matyang’i alisema.