Polisi wakamata raia wa Uganda anayedaiwa kuua mwanadada kwa kumtupa kutoka kwa roshani Nyali

Muhtasari

•Mayanja anadaiwa kuenda mafichoni baada ya kurusha mwanadada wa miaka 25 kutoka kwa roshani ya chumba chake cha malazi mida ya saa tisa asubuhi ya kuamkia Jumatatu.

•Ilibainika kwamba mshukiwa aliwasili nchini mnamo Septemba 1 na walikuwa wamejuana na mwanadada ambaye anadaiwa  kuua kwa kipindi cha siku moja tu.

Suleiman Mayanja
Suleiman Mayanja
Image: TWITTER// DCI

Hatimaye jamaa anayedaiwa kuua mwanadada kwa kumurusha kutoka roshani ya chumba chao cha kulala kilicho katika jengo la Nyali Sunny Side, kaunti ya Mombasa ametiwa mbaroni.

Suleiman Mayanja ambaye ni raia wa Uganda alipatikana akiwa amejificha katika jengo la Nyali Cinemax na kutiwa pingu.

Mayanja anadaiwa kuenda mafichoni baada ya kurusha mwanadada wa miaka 25 kutoka kwa roshani ya chumba chake cha malazi mida ya saa tisa asubuhi ya kuamkia Jumatatu.

Mlinzi ambaye alikuwa analinda jengo lile alisikia mayowe ya mwanamke kutoka hewani kabla  kishindo kikubwa kusikika sekunde chache baadae.

Mlinzi huyo alipokaribia kile alichosikia kikianguka alipigwa na butwa kubwa kuona kuwa ulikuwa mwili wa mwanamke aliyekuwa nusu uchi. Mwili huo ulikuwa umezungukwa na dimbwi la damu.

Wasimamizi wa jengo hilo walipogundua kuwa mwili ule ulikuwa wa mwanadada aliyekuwa ameandamana na Mayanja usiku walienda hadi kwa chumba chake na kupata mlango ukiwa wazi na hakuna yeyote aliyekuwa mle ndani.

Hapo wakapiga ripoti kwa maafisa katika kituo cha Nyali ambao walianzisha msako wa kuwinda mshukiwa.

Kulingana na DCI, Manyaja alikuwa ametuma dereva wa taxi kumchukulia vitu vyake kutoka chumba ambacho alikuwa amehifadhiwa tangu Alhamisi wiki iliyopita.

Dereva yule alipofika chumbani kuchukua vitu vya mshukiwa alikamatwa na polisi na kuhojiwa kuhusu alikokuwa mshukiwa ambaye alimtuma. Dereva huyo aliwaelekeza wapelelezi hadi mafichoni ya Mayanja.

Ilibainika kwamba mshukiwa aliwasili nchini mnamo Septemba 1 na walikuwa wamejuana na mwanadada ambaye anadaiwa  kuua kwa kipindi cha siku moja tu.

Wawili hao walipatana katika baa moja ambapo walijiburudisha kabla ya kuandamana hadi kwa chumba ambacho Mayanja alikuwa amekodishwa.