Jamaa aliyedunga mkewe mara 6 baada ya kumfumania na mwanaume kitandani ajisalimisha Machakos

Muhtasari

•Mutiso ambaye amekuwa akisakwa bila mafanikio tangu atekeleze unyama huo siku ya Alhamisi wiki iliyopita alikuwa ameandamana na ndugu zake wawili wakati alipojisalimisha.

•Majirani ambao walikuwa na ufahamu wa mzozo ulioibuka kati ya wanandoa hao wawili baada ya Mutiso kupata jamaa mwingine akimsaidia majukumu yake ya kitandani walifahamisha polisi mwili ule ulipopatikana.

Pingu
Image: Radio Jambo

Jamaa mmoja anayeaminika kuua mkewe baada ya kumfumania na mwanaume mwingine nyumbani kwake anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Athi River.

Andrew Mutiso Masau 28, ambaye anaripotiwa kudunga mkewe kwa kisu mara sita alijisalimisha kwa polisi mwenyewe siku ya Jumapili mwendo wa alasiri baada ya kuwa mafichoni kwa siku nne.

Mutiso ambaye amekuwa akisakwa bila mafanikio tangu atekeleze unyama huo siku ya Alhamisi wiki iliyopita alikuwa ameandamana na ndugu zake wawili wakati alipojisalimisha.

Mwili wa mkewe Mutiso ulipatikana na wazee wa nyumba kumi ndani ya nyumba yao siku mbili baada yake kukosekana asijulikane alipo.

Majirani ambao walikuwa na ufahamu wa mzozo ulioibuka kati ya wanandoa hao wawili baada ya Mutiso kupata jamaa mwingine akimsaidia majukumu yake ya kitandani walifahamisha polisi mwili ule ulipopatikana.

Wapelelzi kutoka kituo cha Kitengela walifika katika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali kisha kupeleka mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti.

Mutiso anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi leo (Jumatatu) huku uchunguzi wa mwili ukisubiriwa.