Wabakaji na wauaji sugu wakamatwa baada ya kupatikana wakitumia simu ya mhasiriwa wao mmoja

Muhtasari

•Jeremiah Ongati Makambo ,30, Silas  Kipyegon ,24 na Daniel Gatungata walikamatwa siku ya Jumatatu kufuatia uchunguzi wa kina kuhusiana na ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake Ruiru.

•Watatu hao wanaripotiwa kutumia simu ya marehemu kwa kubadilishana hadi walipokamatwa na wapelelezi na kutiwa pingu. 

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Kiambu wanazuilia jamaa watatu wanaoaminika kuwa wanachama wa genge linalobaka na kuua wanawake katika eneo la Ruiru.

Jeremiah Ongati Makambo ,30, Silas  Kipyegon ,24 na Daniel Gatungata walikamatwa siku ya Jumatatu kufuatia uchunguzi wa kina kuhusiana na ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake Ruiru.

Kulingana na DCI, washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Wataalam baada ya kuhusishwa na mauaji ya mwanadada mmoja kutoka eneo hilo.

Washukiwa wanadaiwa kuua kinyama Lovince Njoki mnamo Agosti 23 kisha wakaiba baadhi ya vitu vyake vya thamani ikiwemo simu.

Watatu hao wanaripotiwa kutumia simu ya marehemu kwa kubadilishana hadi walipokamatwa na wapelelezi na kutiwa pingu. 

Simu ya marehemu ambayo wamekuwa wakitumia ilipatikana na inazuiliwa pia ili itumike kama ushahidi mahakamani.

Haya yanajiri takriban wiki mbili tu baada ya mshukiwa mwingine wa ubakaji na mauaji ya wanawake kukamatwa katika eneo hilo la Ruiru.

Paul Magara Morara alikamatwa mnamo Oktoba 14 baada ya kuhusishwa na mauaji ya wanawake watatu na kujeruhi wanne vibaya.

Ilidaiwa kwamba Magara ambaye alikuwa amebandikwa jina 'Mkisii' alikuwa anavizia wanawake mida ya usiku na kuwajeruhi huku akiua wengine kisha kuwatoa chupi zao na kutoroka nazo.

Uchunguzi ulibaini kwamba mnamo mwaka wa 2013 Magara alijiingiza kwa kundi ambalo liliahidi kumlipa kila baada ya kuua mwanamke na kuenda  kuonyesha chupi zao.

Kwa bahati mbaya, mhasiriwa wake mmoja aliyekuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha hospitali ya Kenyatta anaripotiwa kufariki kutokana na majeraha.