Usajili wa wapiga kura wapya, asilimia 25.3 pekee wajisajili

Asilimia 25.3 ya lengo la tume hiyo ndiyo iliyoweza kuafikiwa.

Muhtasari

• IEBC ilikuwa inalenga kusajili wapiga kura wapya angalau milioni sita katika kipindi cha mwezi mmoja ambacho shughuli ya usajili ilifanyika.

• Tume pia imetangaza kuwa wapiga kura 421, 057 walibadilisha vituo vyao vya kupiga kura katika kipindi hicho.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) imetangaza matokeo ya shughuli ya hivi punde ya usajili wa wapiga kura ambayo ilitamatika siku ya Ijumaa wiki iliyopita.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya wanahabari siku ya Jumanne, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema wapiga kura wapya 1,519, 294 ndio waliyosajiliwa kufikia Novemba 5.

IEBC ilikuwa inalenga kusajili wapiga kura wapya angalau milioni sita katika kipindi cha mwezi mmoja ambacho shughuli ya usajili ilifanyika. Hata hivyo, ni asilimia 25.3 ya lengo la tume hiyo iliyoweza kuafikiwa.

Tume hiyo italinganisha data za kibayometriki za wapiga kura wapya na wapiga kura 19, 668, 968 ambao tayari walikuwa kwenye sajili ya wapiga kura ili kuhakikisha hakuna majina yanayojirudia. Pia data za wapiga kura walioaga dunia zitafutwa.

Tume pia imetangaza kuwa wapiga kura 421, 057 walibadilisha vituo vyao vya kupiga kura katika kipindi hicho.

Usajili wa wapiga kura wanaoishi nje ya  mipaka ya Kenya utang'oa nanga  mnamo Desemba 6 na kuendelea kwa siku 15 hadi Desemba 20.