Uhuru aagiza kuimarishwa usalama kote nchini

Muhtasari

• Rais aliagiza kuimarishwa kwa doria kutokana na kudorora kwa hali ya usalama katika kanda hii.

• Rais Kenyatta alitoa agizo hilo wakati akiongoza mkutano wa baraza la kitaifa la usalama.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ameagiza idara za usalama kuimarisha usalama kote nchini.

Rais kupitia taarifa siku ya Ijumaa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na msemaji wa Ikulu Kanze Dena, aliagiza kuimarishwa kwa doria kutokana na kudorora kwa hali ya usalama katika kanda hii.

Rais Kenyatta alitoa agizo hilo wakati akiongoza mkutano wa baraza la kitaifa la usalama.

Eneo la Africa mashariki limekuwa likishudia changamto sa kiusalama hasa kufuatia mapigano ambayo yanaendelea nchini Ethiopia na hali tete nchini Sudan bila kusahau mataifa ya Sudan Kusini na Somalia ambaya hayana uthabiti.

Agizo hili la rais pia linajiri siku chache tu baada ya serikali kutangaza zawadi ya jumla ya shilingi milioni 50 kwa yeyote atakaye saidia kunaswa kwa washukiwa watano wa ugaidi akiwemo Elgiva Bwire anayeaminika kutoroka punde tu alipoachiliwa kutoka jela.

Washukiwa wa ugaidi wanaosakwa

  1. Elgiva Bwire Oliacha aka Seif Deen Mohamed aka Japhar aka Japhel Okuku aka Abu Muadh

Aliachiliwa kutoka gereza la Kamiti tarehe 28/10/2021 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 kwa kosa ka kushiriki shughuli za kigaidi.

Kulingana na taarifa ya DCI  Elgiva alikuwa ameahidi kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. Alienda mafichoni punde tu alipoachiliwa na inaaminika anapanga kutekeleza mashambulizi. Idara ya polisi inataka mtu yeyote aliye na ripoti kumhusu kujulisha polisi.

  1. Salim Rashid Mohamed aka Chotara aka Turki

Salim alikuwa ameachiliwa kwa dhamana na anaaminika kujiunga na kundi la Daesh, kundi la kigaidi linaloendesha shughuli zake nchini Musumbiji.

Ni mzaliwa wa Mombasa na amehusishwa sana na visa kadhaa vya uhalifu. Kulingana na ripoti za kijasusi Salim anapanga kurejea nchini kutekeleza mashambulizi ya kigaidi.

  1. Birigi Abdikadir Haila

Kulingana na DCI Birigi amejiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia hivi majuzi. Ni mzaliwa wa eneo la Manyatta, Moyale kaunti ya Mandera. Polisi wanasema amejihami kwa silaha na ni hatari na wananchi wametahadharishwa kumhusu.

  1. Muhammad Abubakar alia Minshawary

Anashukiwa kujiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia. Ni mzaliwa wa eneo la Kibokoni, Old town  kaunti ya Mombasa. Wananchi wametahadharishwa kumhusu.

  1. Trevor Ndwiga aka idriss Jamal

Trevor ambaye alikuwa ameachiliwa kwa dhamana anaaminika kujiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia.Anatoka eneo la Hamza, kaunti ndogo ya Makadara katika kaunti ya Nairobi.

Idara ya polisi ilitangaza kwamba watano hao ni hatari na wanapanga kutekeleza mashambulizi humu nchini.