Bweni lateketea katika shule ya upili ya wasichana ya Kerugoya, wanafunzi kadhaa wakimbizwa hospitali

Muhtasari

•Inaripotiwa kwamba baadhi ya wasichana walivuta moshi wakati bweni hilo lilikuwa linateketea na kufuatia hayo wakakimbizwa hospitalini ili kupokea matibabu ya dharura.

•Jioni hiyo hiyo ya Jumapili, bweni lingine liliteketea katika shule ya upili ya wavulana ya Jamhuri iliyo jijini Nairobi.

Shule ya upili ya wasichana ya Kerugoya
Shule ya upili ya wasichana ya Kerugoya
Image: amedleyadventure.blogspot.com

Takriban wanafunzi 40 kutoka shule ya upili ya wasichana ya Kerugoya walikimbizwa  hospitalini baada ya kuvuta moshi wakati bweni moja lilishika moto na kuteketea.

Bweni moja katika shule hiyo iliyo katika kaunti ya Kirinyaga liliteketea vibaya mwendo wa jioni na mali yenye thamani kubwa kuharibiwa.

Inaripotiwa kwamba baadhi ya wasichana walivuta moshi wakati bweni hilo lilikuwa linateketea na kufuatia hayo wakakimbizwa katika hospitali ya Kerugoya Level 5 ili kupokea matibabu ya dharura.

Wanafunzi hao walihudumiwa na kuruhusiwa kurudi shuleni.

Wazazi wengi walijumuika nje ya shule hiyo kujua hali ya watoto wao baada ya kupokea ripoti hizo za kuhuzunisha.  Chanzo cha moto ule bado hakijabainika.

Jioni hiyo hiyo ya Jumapili, bweni lingine liliteketea katika shule ya upili ya wavulana ya Jamhuri iliyo jijini Nairobi.

Bweni hilo ambalo liliteketea mwendo wa saa mbili usiku linaripotiwa kuwa malazi ya wanafunzi 300.

Wazima moto pamoja na polisi walifika katika eneo la tukio punde baada ya kupokea ripoti. Hata hivyo, chanzo cha moto ule bado hakijabainika.

Haya yanajiri huku visa vya uchomaji shule vikiwa vimekithiri nchini. 

Zaidi ya shule 20 zimeripoti visa vya moto katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mapema mwezi huu waziri wa masomo George Magoha alitangaza wazazi watagharamia hasara zote ambazo zitapatikana kutokana na matukio yale.