Jamaa adunga mpenziwe kwa kukataa ombi lake la ndoa kisha kujitia kitanzi Bungoma

Muhtasari

• Inadaiwa marehemu alimshutumu msichana huyo kwa kumtorosha pesa zake na kukataa ombi lake la kutaka kumuoa.

•Ndugu ya marehemu alisema kakake ni baba wa watoto wanne huku akifichua mke wake wa kwanza alimuacha kwa kosa la kuenda nje ya ndoa.

•Mwili wa marehemu ulichukuliwa na polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Bungoma ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Wakaazi wa kijiji cha Rurare, wadi ya Musikoma eneo bunge la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma waliamkia tukio la kushtua asubuhi ya Jumatatu  ambapo  jamaa aliyetambulishwa kama Evans Wanjala, 34, alipatikana akiwa amejitoa uhai baada ya msichana aliyekuwa akichumbiana kukataa ombi lake la kutaka kumuoa.

 Kulingana na uchunguzi wa awali, marehemu alivamia kwanza nyumbani kwa msichana huyo na kumchoma kisu tumboni kabla ya kujitoa uhai.

 Inadaiwa marehemu alimshutumu msichana huyo kwa kumtorosha pesa zake na kukataa ombi lake la kutaka kumuoa.

Akiongea na KNA, kaka wa marehemu, Fidelis Mechumo, alithibitisha mapenzi kati ya marehemu kakake na Juliet Makokha, 29, kwa miezi tisa iliyopita.

“Kama angeweza kunishirikisha kwa yale anayopitia ningeweza kumshauri, ni bahati mbaya kwamba amejiua, ni ombi langu la unyenyekevu kwamba wale walio katika masuala ya mapenzi watafute mwongozo sahihi wa njia ya kwenda mbele iwapo hawataelewana na wapenzi wao. " alisema.

Pia alisema marehemu ni baba wa watoto wanne huku akifichua mke wake wa kwanza alimuacha kwa kosa la kutembea nje ya ndoa.

 "Mke wa kaka yangu alimwacha kwa sababu ya kujihusisha na Juliet lakini njiani marehemu alikosana naye baada ya kumlaghai zaidi ya Sh.50, 000," aliongeza.

Kamanda wa Polisi wa Bungoma Kusini, Benjamin Kimwele alithibitisha kisa hicho.

Alieleza kuwa marehemu alikuwa na ugomvi na mpenzi wake katika nyumba ya mpenzi huyo kabla ya kukamata kisu cha jikoni na kumchoma mara kadhaa tumboni. Baada ya kubaini kuwa binti huyo alikuwa amepoteza fahamu, marehemu alitoweka lakini alipatikana akining’inia juu ya mti ulikouwa nyuma ya nyumba yake huku akiwa na kamba ya manila shingoni.

Kimwele aliongeza kuwa mwanamke huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma ambako amelazwa akiwa katika hali mahututi.

Mwili wa marehemu ulichukuliwa na polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Bungoma ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

“Tukio la namna hii ni ukiukwaji wa haki za binadamu na sisi kama polisi hatutafurahia vitendo hivyo. Walio katika masuala ya mapenzi wanapaswa kutafuta mwongozo na ushauri kutoka kwa mamlaka husika kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho,” alisema.

(Utafsiri wa Samuel Maina)