Wanafunzi 5 wa kike watiwa mbaroni kwa kuteketeza bweni Machakos

Muhtasari

•Wanafunzi waliokamatwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uchomaji yanayowakabili.

 

Pingu
Image: Radio Jambo

Wapelelezi katika kaunti ya Machakos wamewatia mbaroni wanafunzi watano wa shule ya upili ya wasichana ya Maasani baada ya kuwahusisha na tukio la moto ambao uliteketeza bweni moja  shuleni humo mnamo Novemba 5.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na idara ya polisi, watano hawa walikamatwa baada ya uchunguzi wa DCI kubaini walihusika katika uteketezaji wa bweni hilo.

Wanafunzi waliokamatwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uchomaji yanayowakabili.

Mali yenye thamani ya milioni nne iliharibiwa katika tukio hilo lililotokea mapema mwezi huu.

Huduma ya polisi nchini (NPS) imetahadharisha kuwa hali ya kuwa mwanafunzi haizuilii yeyote dhidi ya kuadhibiwa kisheria.

"Uchomaji ni hatia mbaya na mtu anaweza kuadhibiwa kwa kuhukumiwa kifungo cha maisha. Tunaomba wazazi na walimu waendelee kukumbusha wanafunzi malipo ya uhalifu wowote. NPS itachukua hatua kali kwa wahalifu wote na wanaoshirikiana nao kama vile wanaouza petroli inayotumika kuchoma shule" NPS imesema.

NPS imehimiza wapelelezi kuchunga visa vya uchomaji shule kwa kina na kuhakikisha wanaopatikana na hatia wameshtakiwa ifaavyo.