Ruto adai uwepo wa Raila kwenye Jubilee ulisambaratisha chama hicho

Muhtasari
  • Naibu wa rais Dr. William Ruto Jumatano,  kaunti ya Garissa akiwahotubia wakazi aliwaeleza kiini cha  chama kilichoko mamlakani, Jubilee kusambaratika
Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: twitter/DP

Naibu wa rais Dr. William Ruto Jumatano,  kaunti ya Garissa akiwahotubia wakazi aliwaeleza kiini cha  chama kilichoko mamlakani, Jubilee kusambaratika.

Ruto alisema ujio wa waziri  mkuu wa zamani  Raila Odinga katika chama chao cha Jubilee kulifanya  washindwe kuafikia  ajenda kuu za chama hicho.

"Tulitembelewa na watu wenye kisirani, wakatuletea kisirani kwenye chama, wakasambaratisha serikali yetu. wakakoroga mpango wetu wa Big 4 wakatuletea reggae" Ruto alisema.

 

Ruto alisisitiza kuwa kusimama kwa  Raila kwenye kiti cha urais  unasukumwa na matajiri wachache ambao wanalinda biashara zao kwa gharama ya Wakenya maskini

"Watu wachache  kwa sababu  wana akaunti nono za benki kwa kiburi chao, walipanga njama ya kutuamulia nani awe rais wetu. Wameandaa mahojiano na kutuwekea wanayemtaka awe Rais wa taifa hili" Ruto alisema

Aliendelea kusema wenye mpango wa kusimamisha viongozi watakabiliwa na hatima sawa na ile ya BBI ambayo alidai  ilikuwa mfumo usioweza kukomboa mwananchi wa kawaida.

"Sasa wamebuni mpango mwingine wa kubadilisha sheria ili wagawanye watu wa Kenya katika vyama vya vijiji vya kikabila ili waweze kumweka rais kibaraka ambaye atashughulikia maslahi yao,” Ruto alidai. Alifichua kuwa mswada wa sasa wa vyama vya kisiasa (marekebisho), 2021 ni sehemu ya mpango mpana wa kugawanya Wakenya katika vyama vya kanda na kumsaidia mkuu wa ODM kutwaa mamlaka" Ruto alikuwa akizungumzia mswada uliokuwa umepelekwa bungeni.