Jamaa watatu watiwa mbaroni kwa kumteka nyara kijana mmoja Githurai

Muhtasari

•Mhasiriwa alipofika pale alimpata mke wa boma ile pekee yake kisha mumewe akaingia muda mfupi baadae akiwa ameadamana na wanaume watatu na kumshtumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.

Pingu
Image: Radio Jambo

Jamaa watatu walitiwa mbaroni siku ya Jumanne kwa kumteka nyara kijana mwenye umri wa miaka 23 katika eneo la Githurai na kudai familia yake shilingi laki tatu ili kumwachilia huru.

Dickson Mwendwa 24, Robert Kioko 23 na Philip Kilonzi walivimiwa na kukamatwa  na wapelelezi wa DCI katika chumba ambacho walikuwa wamemficha mhasiriwa wao.

Kulingana na DCI, mhasiriwa alikuwa amesafiri kutoka eneo la Mwingi Mashariki kwenda Githurai kutembelea wanandoa ambao wametoka eneo moja naye

Mhasiriwa alipofika pale alimpata mke wa boma ile pekee yake kisha mumewe akaingia muda mfupi baadae akiwa ameadamana na wanaume watatu na kumshtumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.

Washukiwa walimpora mhasiriwa na kuchukua shilingi elfu tano alizokuwa nazo kabla yya kumtoa nje ya nyumba hiyo na kumpeleka kwa chumba kingine kilichokuwa wazi.

Mhasiriwa alilazimishwa kupigia wanafamilia wake na awaarifu wachange Sh300,000 huku wakimtishia kwa matokeo mabaya iwapo wangekosa kufanya vile.

Baba ya mhasiriwa aliwafahamisha wapelelezi kuhusu kilichokuwa  kimemtendekea mwanawe na hapo wakaanzisha msako mkali.

Wapelelezi walifanikiwa kupata chumba ambacho washukiwa walikuwa wamemuweka mhasiriwa  na kuwatia pingu.

Mhasiriwa ambaye alikuwa amevuliwa nguo na kujeruhiwa usoni aliokolewa huku washukiwa wakipelekwa kizuizini kusubiri kushtakiwa.