Sifuna ajitokeza kuzima uvumi kuwa alifariki baada ya kupigwa na mwanasiasa mwenzake

Sifuna ambaye alionekana wazi kuwa buheri wa afya aliyadhihaki madai hayo mabaya.

Muhtasari

•Sifuna amejitokeza kuuzika uvumi kuwa aliaga dunia kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyopata baada ya kushambuliwa na mwanasiasa mwenzake.

•Katibu huyo mkuu wa chama cha ODM aliwakashifu watu wenye chuki ambao wamekuwa wakimuombea mabaya maishani.

Mgombea useneta wa Nairobi kwa tiketi ya ODM Edwin Sifuna
Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Mgombea useneta wa Nairobi kwa tiketi ya ODM Edwin Sifuna hatimaye amejitokeza kuuzika uvumi kuwa aliaga dunia usiku wa kuamkia Jumapili kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyopata baada ya kushambuliwa na mwanasiasa mwenzake.

Kupitia kanda fupi ya video ambayo alipakia Jumapili asubuhi kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Sifuna ambaye alionekana wazi kuwa buheri wa afya aliyadhihaki madai hayo mabaya.

"Nakuja moja kwa moja kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha  City. Naambiwa kule Facebook mmenipiga usiku, mkanipeleka Nairobi Hospital nikalazwa ambapo nilifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa," Sifuna alisema.

Katibu huyo mkuu wa chama cha ODM aliwakashifu watu wenye chuki ambao wamekuwa wakimuombea mabaya maishani.

"Miaka tano unaombea mtu apigwe na hapigwi.  Si uombe maombi ingine hiyo imekataa!" Alisema.

Katika video hiyo walikuwepo pia mgombea ubunge wa Langata Felix Odiwour almaarufu Jalango, aliyekuwa spika wa Nairobi Beatrice Elachi na Bw Wanguru Mwangi.

Ili kuthibitisha kuwa kwa kweli  ni mzima wa afya, Sifuna alidokeza kwamba angetumia siku nzima kwenye kampeni za Azimio la Umoja-One Kenya ndani ya Nairobi.

"Leo tuko siku ya pili ya ziara ya Baba na Mama. Tuko kwa Jalas kule Lang'ata kisha tuingie Kibra na Embakasi Kusini...,"

Sifuna anadaiwa kushiriki makabilianio makali na mgombea wa kiti cha MCA cha Kileleshwa Robert Alai wakati wa mkutano wa kisiasa jijini Nairobi siku ya Jumamosi.

Video ambayo ilienezwa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonyesha mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga  akimwagiza Alai kukoma baada ya kudaiwa kumpiga Sifuna.

"Alai, Alai, Alai, Alai!.. Kama unataka..  Tafadhali! Tafadhali, Tafadhali!" Raila alisikika akisema kwenye video hiyo.

Baadae uvumi ulienezwa kwamba katibu mkuu wa ODM alikimbizwa hospitali kutokana na majeraha mabaya alipata kwenye makabiliano hayo.