Shirika la Save The Children lazindua mpango unaolenga watoto katika mazingira magumu

Mpango huo utagharimu jumla ya dola za Marekani milioni 26

Muhtasari

• Takriban watu milioni 4.1 wakisemekana kukabiliwa na uhaba wa chakula kulingana na ripoti ya tathmini ya usalama wa chakula kati ya mwezi Machi na Juni.

Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Kenya na Madagascar Yvonne Arunga na Katibu wa Huduma za Watoto kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Huduma za Watoto Shem Nyakutu wakati wa uzinduzi wa mpango kulinda watoto. 29/7/2022.
Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Kenya na Madagascar Yvonne Arunga na Katibu wa Huduma za Watoto kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Huduma za Watoto Shem Nyakutu wakati wa uzinduzi wa mpango kulinda watoto. 29/7/2022.

Shirika la Save the Children limezindua mkakati kabambe unaolenga zaidi ya watoto milioni moja waliotengwa na wanaoishi katika mazingira magumu nchini Kenya, katika miaka mitatu ijayo.

Mpango huo ambao ulizinduliwa siku ya Ijumaa utateketezwa katika kipindi kati ya mwaka 2022-2024 utagharimu jumla ya dola za Marekani milioni  26; fedha ambazo zitapatikana kupitia raslimali za humu nchini na kimataifa.

Mpango huu wa malengo ya miaka mitatu unachangia moja kwa moja katika mkakati wa kimataifa wa shirika la Save the Children na unaendeleza azma ya shirika hilo ya mwaka 2030 ya kuhakikisha watoto wanaishi, wanasoma na wanalindwa na inaangazia zaidi afya na lishe, elimu, ujuzi wa kiufundi kwa vijana na hali zao za kibinadamu.

Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Kenya na Madagascar Yvonne Arunga.
Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Kenya na Madagascar Yvonne Arunga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkakati huo, Mkurugenzi wa shirika la Save The Children nchini Kenya na Madagascar Yvonne Arunga, alisema mkakati huo unalenga watoto waliotengwa na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi.

"Tunataka watoto wetu, wanapozaliwa, wawe na nafasi kubwa zaidi ya kuishi. Kwa sasa, tunapoteza watoto wengi sana wakati wa kuzaliwa na katika miaka ya mwanzo, kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika kama vile nimonia, kuhara, malaria na utapiamlo,” Yvonne Alisema. 

Katibu wa Huduma za Watoto kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Huduma za Watoto Shem Nyakutu alipongeza shirika la Save the Children kwa mpango huo wa miaka mitatu na kubainisha kuwa ni mpango kabambe na wenye kuleta mabadiliko ambao utalinda haki za watoto nchini Kenya na kuwasaidia kufikia uwezo wao kamili.  

Akibainisha kuwa watoto ni takribani asilimia 52 ya watu wote, alisema wengi wao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kihisia na kingono, kutelekezwa na wazazi, ajira ya watoto na ukiukwaji wa haki zao zinginezo.  Alisema kuwa ushirikiano na mashirika yenye lengo sawia kama vile Shirika la Save the Children, utachangia pakubwa katika kulinda haki za watoto.  

Katibu wa Huduma za Watoto kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Huduma za Watoto Shem Nyakutu.
Katibu wa Huduma za Watoto kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Huduma za Watoto Shem Nyakutu.

Mpango huo unazinduliwa wakati ambapo Kenya inakabiliwa na hali mbaya ya ukame kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, huku takriban watu milioni 4.1 wakisemekana kukabiliwa na uhaba wa chakula kulingana na ripoti ya tathmini ya usalama wa chakula kati ya mwezi Machi na Juni.

Kulingana na tathmini hiyo jumla ya watoto 942,000 chini ya miaka mitano wanahitaji matibabu ya dharura ya utapiamlo uliokithiri huku wanawake wajawazito na wanaonyonyesha 134,000 pia wakikosa lishe bora.