Kamanda wa polisi atekwa nyara na kupokonywa bunduki

Fredrick Siundu alivamiwa na watu wawili waliokuwa wamejihami alipokuwa akifungua lango nyumbani kwake.

Muhtasari

• Polisi walisema alilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Toyota Wish, ambalo usajili wake haujulikani, na kupelekwa eneo la Mau Narok.

• Sababu ya kutekwa kwake haikujulikana mara moja lakini watekaji nyara hao walionekana katika eneo la Tipis.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Narok Central Fredrick Shiundu. Picha: HISANI
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Narok Central Fredrick Shiundu. Picha: HISANI

Kamanda wa polisi aliokolewa Jumatano asubuhi baada ya kutekwa nyara na kupokonywa bunduki nyumbani kwake na watu waliyokuwa wamejihami katika Kaunti ya Narok.

Afisa mkuu wa polisi wa Narok Central Fredrick Siundu Kinaibei alivamiwa na watu wawili waliokuwa wamejihami alipokuwa akifungua lango nyumbani kwake usiku wa manane Jumatano.

Polisi walisema alilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Toyota Wish, ambalo usajili wake haujulikani, na kupelekwa eneo la Mau Narok.

Mkewe alifahamisha polisi kituoni kwamba afisa huyo mkuu alikuwa ametekwa nyara kwa njia ya simu.

Polisi walifika nyumbani kwake mara moja na kugundua kuwa alitekwa nyara wakati akifungua lango.

Gari lake lilipatikana nje likiwa bado linanguruma na simu yake ikiwa ndani.

Sababu ya kutekwa kwake haikujulikana mara moja lakini watekaji nyara hao walionekana katika eneo la Tipis takriban kilomita 77 kutoka eneo la tukio na kupelekea msako mkali katika eneo hilo.

Alipatikana akiwa ametelekezwa katika eneo la Tipis karibu na mto saa tisa unusu asubuhi akiwa bado amevalia sare za polisi.

“Walimtupa katika eneo la Tipis na kuokolewa na mlinzi. Hakujeruhiwa wakati wa tukio hilo,” polisi walisema. Bunduki yake ambayo ilikuwa na risasi 14 iliibwa.

Kamanda wa polisi wa Narok Kizito Mutoro alisema wanachunguza tukio hilo.

"Tunawawinda wanaume walioiba silaha hiyo na pia tunachunguza nia yao," alisema.