Shule ya Upili ya Wavulana ya Butere yafungwa baada ya hofu ya kipindupindu

Tofauti na Mukumu ni kwamba Mukumu wanafunzi walikuwa wakichukua muda mrefu kupona.

Muhtasari

• Wanafunzi walioathiriwa walitibiwa katika hospitali ya Butere level 4 na kuruhusiwa kwenda nyumbani wakiwa katika hali thabiti. 

Image: HISANI

Shule ya upili ya wavulana ya Butere katika kaunti ya Kakamega imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia hofu ya mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu. 

Wanafunzi wote walitumwa nyumbani baada ya wanafunzi 100 kulalamikia maumivu ya tumbo na kuendesha. 

“Ndugu mzazi/Mlezi, hii ni kukujulisha kuwa mwanao ametumwa nyumbani kutokana na mkurupuko wa maradhi ya tumbo na kuendesha,” barua ya shule ilisema.

 "Mara tu idara ya afya ya umma itatupa ripoti iwapo shule ni salama kwa mtoto wako, tutawakumbusha tena. Tuvumilie, Mwalimu Mkuu." 

Wanafunzi walioathiriwa walitibiwa katika hospitali ya Butere level 4 na kuruhusiwa kwenda nyumbani wakiwa katika hali thabiti. 

Mkurugenzi wa Elimu wa Kanda ya Magharibi Jared Obiero, hata hivyo, alikanusha kuwa shule hiyo ilikuwa imefungwa. Alidai kuwa masomo yalikuwa yanaendelea shuleni. 

Obiero alisema kuwa wanafunzi 80 wa kidato cha kwanza waliolalamikia maumivu ya tumbo walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. 

"Ni kama walikula kitu ambacho kilisababisha maumivu ya tumbo kwa sababu unajua wale wa kidato cha kwanza wanakula mwisho. Walitibiwa na kupewa antibiotics. Hakuna sababu ya kuhofia,” Obiero alisema kwenye simu. 

"Tunachunguza ili kubaini sababu ya maumivu," alisema. 

Alipuuzilia mbali ripoti kuwa shule hiyo ilikuwa imefungwa kutokana na hofu ya kipindupindu. 

"Tofauti na Mukumu ni kwamba Mukumu wanafunzi walikuwa wakichukua muda mrefu kupona," aliongeza. 

Kisa hiki kinajiri siku moja tu baada ya Shule ya Upili ya Wasichana ya Sacred Heart Mukumu katika kaunti hiyo kufungwa kwa mwezi mmoja kufuatia vifo vya wanafunzi wawili kutokana na maradhi ya tumbo. 

Wanafunzi 124 katika shule hiyo walilazwa katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega Jumatano iliyopita kutokana ugonjwa wa kuendesha. 

Madaktari walisema wanafunzi hao walimbukizwa kupitia kwa maji au chakula.