Jamaa akamatwa kwa madai ya kumuua mkewe na kuchoma mwili wake

Polisi walikuta mwili wa marehemu ukiwa bado unawaka moto na umechomeka kabisa.

Muhtasari

•Titus Nderitu  anadaiwa kumuua mpenziwe nyumbani kwao kabla ya kutumia gari lake kusafirisha maiti hadi kijiji cha Pesi alikochomea mwili.

•Awali polisi walikuwa wakichukulia kisa hicho kama kisa cha utekaji nyara.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi huko Nyandarua wanamzuilia mwanamume mmoja kwa tuhuma za kumuua mpenziwe kikatili,na kuchoma mwili wake.

Kulingana na ripoti ya polisi, Titus Nderitu Gichohi, anadaiwa kumuua mpenziwe nyumbani kwao kabla ya kutumia gari lake kusafirisha maiti hadi kijiji cha Pesi, eneo bunge la Ndaragua, ambapo inadaiwa aliiuchoma moto ili kuharibu ushahidi wowote ambao ungemhusisha na mauaji.

''Uchunguzi wa matukio hayo unaonyesha kuwa mwathiriwa aliuawa ndani ya nyumba yake na mwili wake kuhamishwa hadi eneo la nyingine ambapo mshukiwa aliuchoma katika juhudi za kuharibu ushahidi,” Ripoti ya polisi imesema.

Awali polisi walikuwa wakichukulia kisa hicho kama kisa cha utekaji nyara kabla ya wakaazi wa eneo hilo kutoa taarifa kwamba walikuwa wameona gari la marehemu nyumbani kwa Gichohi.

Hili liliwafanya wapelelezi kuzuru eneo la tukio, ambapo walikuta mwili wa marehemu ukiwa bado unawaka moto na kuchomeka kabisa.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Aberdare Charles Rukwaro, mshukiwa hakuwa katika eneo la tukio wakati huo lakini inasemekana alikamatwa na polisi eneo la Kasarani alipokuwa akijaribu kutoroka.

Mwili wa marehemu umehamishiwa katika hospitali ya Nyahururu kaunti ya Laikipia.