Majambazi 3 wapoteza maisha katika majibizano makali ya risasi na polisi Mombasa Road

Wenzao watatu walifanikiwa kutoroka na majeraha mabaya ya risasi

Muhtasari

•Genge hilo lilikuwa limetoka tu kufanya wizi na walikuwa wakielekea kwenye misheni nyingine ya wizi  kando ya Mombasa  Road.

•Wapelelezi waliwaamuru majambazi hao kusimama lakini wakakaidi amri na kuanzisha mashambulizi ya risasi.

Majambazi watatu walipoteza maisha yao katika makabiliano makali ya risasi na polisi Mombasa Road Jumanne jioni
Majambazi watatu walipoteza maisha yao katika makabiliano makali ya risasi na polisi Mombasa Road Jumanne jioni
Image: DCI

Majambazi watatu walifariki na wenzao watatu kutoroka na majeraha ya risasi katika makabiliano makali na wapelelezi wa DCI yaliyotokea Jumanne jioni katika eneo la Imara Daima, jijini Nairobi. 

Genge hilo lilikuwa limetoka tu kufanya wizi na walikuwa wakielekea kwenye misheni nyingine ya wizi  kando ya Mombasa  Road wakati maafisa walipowapata.

Kitengo cha DCI kimesema mtu asiyejitambulisha aliwafahamisha kuhusu wizi ambao ulikuwa umefanyika katika eneo moja la Mombasa Road na hapo wakachukua hatua na kuweka shambulizi.

"Dakika chache baadaye, watu sita wenye kutiliwa shaka waliofanana na maelezo yaliyotolewa na mpiga simu aliyejawa na wasiwasi walikaribia gari la wapelelezi, lililoegeshwa  kwenye ukingo wa barabara waliyokuwa wakitumia," Taarifa ya DCI ilisoma.

Wapelelezi waliwaamuru majambazi hao kusimama lakini wakakaidi amri na kuanzisha mashambulizi ya risasi.

Kuona hivyo, wapelelezi wale walitoa bunduki zao pia na kuanza kufyatua risasi kuelekeza  upande wa majambazi wale.

"Kufuatia majibizano hayo ya risasi ya Jumanne jioni, bunduki aina ya barreta pistol nambari 1999667 CAT 5802 iliyokuwa na risasi nne za 9mm calibre, bastola moja bandia, simu moja ya mfukoni, laptop moja aina ya HP, nyundo moja, panga moja la Somalia na simu sita za aina mbalimbali zilipatikana kutoka kwa majambazi hao," DCI imesema.

Mwanaume mmoja mwenye asili ya Kihindi aliweza kutambua vitu vilivyopatikana na majambazi hao kuwa vyake.

Miili ya majambazi wanne waliouawa ilipelekwa katika City Mortuary huku msako wa wenza wanne waliotoroka ukiendelea.