Newcastle wakanusha tetesi za kumsaini Ronaldo mwezi Juni mwaka huu kutoka Al Nassr

Kocha Eddie Howe alisema madai hayo ni ya uongo huku akimtakia Ronaldo mema katika changamoto yake mpya Saudia.

Muhtasari

• Ronaldo aliramba dili nono baada ya kusaini mkataba wa miaka 2 na Al Nassr, ambao utamweka timuni hapo hadi mwaka 2025.

• Mchezaji huyo atakuwa anatia mfukoni kitika cha pauni milioni 173 kwa mwaka.

Ronaldo na kocha Howe
Ronaldo na kocha Howe
Image: Instagram

Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Christiano Ronaldo Jumanne usiku alitambulishwa rasmi kama mchezaji wa Al Nassr inayoshiriki ligi ya Saudi Arabia.

Wakati wa kutambulishwa kwake, Ronaldo alisema kuwa yeye na soka la barani Ulaya wamemalizana huku akijipiga kifua kuwa anaondoka Ulaya akiwa ameshinda kila taji maarufu barani humo.

Baada ya kutambulishwa kwake, minong’ono mingi ilizungumziwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi walisema kuwa katika mkataba wake, Newcastle ambayo pia inamilikiwa na raia wa Saudia ina nafasi ya kumuendea katika dirisha la majira ya joto la uhamishaji wa wachezaji.

Kulingana na mwanahabari wa masuala ya soka Fabrizio Romano, kocha wa Newcastle Eddie Howe alikanusha kuwepo kwa kipengele hicho huku akisema kuwa wanamtakia Ronaldo kila la kheri katika changamoto yake mpya kwenye mataifa ya Mashariki ya kati.

“Tunamtakia Ronaldo kila la kheri katika changamoto yake mpya, lakini hakuna ukweli wowote katika dhana hiyo, si kweli kabisa kuwa tutamuendea mwezi Juni, hakuna kipengele kama hicho kwenye mkataba wake,” Howe alisema mara pindi baada ya kumalizika kwa mechi iliyokutanisha Newcastle na viongozi wa ligi ya Premia, Arsenal.

Howe ameiongoza Newcastle na hu ndio msimu ambao timu hiyo imekuwa na mwanzo wa kufana katika kuweka matumaini yao hao kwenye ligi ya Premia huku mpaka sasa baada ya mechi 19, timu hiyo inashikilia nafasi ya tatu na pointi 34, alama 9 tu nyuma ya viongozi wa jedwali, Arsenal.