"Ni mchoyo wa kutoa pesa, ataanguka!" mpiga kura amlipua Mbunge wa Embakasi Magharibi

Muhtasari

• "Huyu jamaa anaita watu mkutano anawapa mkate na soda kutoka duka lake huko Umoja one. Siasa ya Nairobi ni pesa Rafiki yangu,” mpiga kura huyo alimshauri Theuri.

Mpiga kura Ian Kyalo na mbunge wa Embakasi West, George Theuri
Mpiga kura Ian Kyalo na mbunge wa Embakasi West, George Theuri
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Magharibi George Theuri Jumatatu alijipata katika majibizano makali na mpiga kura mmoja aliyekuwa anadai kwamba mbunge huyo alikuwa na nafasi kubwa sana ya kushinda kiti hicho cha ubunge kwa mara ya tatu mtaliwa, lakini kwa sababu ya uchoyo na ubahili wake wa kutoa pesa kwa wapiga kura basi kiti hicho huenda kitamponyoka.

Mfuasi huyo kwa jina Ian Kyalo ambaye pia anajiongeza kama mmoja kati ya washirika wakubwa wa chama cha UDA kinachoongozwa na naibu rais William Ruto aliamua kumpasha mbunge George Theuri katika ukurasa wake wa facebook akimtaja kuwa bahili na mwanasiasa asiye na pesa.

Kulingana na Kyalo, siasa za Nairobi zinahitaji mtu ako na pesa na iwapo mwanasiasa hana pesa basi ni moja kwa moja amejikatia tiketi ya kujiandaa kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Alidai kwamba mbunge huyo anaita watu mkutano na kuwapa mkate na soda pekee.

“George Theuri angeshinda ubunge wa Embakasi Magharibi kwa mara ya tatu mtawaliwa kupitia tiketi ya UDA lakini sasa shida huyu jamaa ni bahili. Huyu jamaa anaita watu mkutano anawapa mkate na soda kutoka duka lake huko Umoja one. Siasa ya Nairobi ni pesa Rafiki yangu,” aliandika Kyalo.

Maneno haya ni kama hayakuenda vizuri na mbunge huyo ambaye aliamua kuweka uheshimiwa pembeni japo kwa sekunde kadhaa na kuamua kuyaoga baada ya kuyavulia. Alimjibu mfuasi huyo na wakati huo huo akadokeza kukanusha madai ya kumiliki duka lililotajwa na Kyalo.

“Kyalo ulisikia niko na duka ama unaniconfuse na uncle yako wa ocha,” Theuri alijibu mipigo.

Kyalo aliyeonekana kumlemea mbunge Theuri katika safu zote za ukabaji na ushambuliaji alimfunga mbunge wake kwa bao la dakika za mazidadi ambapo alimtaka kuwa makini sana anapomjibu kwani yeye ni mwanachama wa UDA na vile vile ajenti wa kituo cha kupigia kura.

“George Theuri, mimi ni mpiga kura eneo bunge la Embakasi Magharibi, nimejiandikisha kama mwanachama wa UDA na pia mimi ni ajenti katika kituo cha kupiga kura. Kwa hiyo kuwa makini sana unaponijibu na badilisha mbinu za kampeni zako kaka,” Kyalo aligongelea msumari wa mwisho katika jeneza la Theuri.

Facebook screenshot
Facebook screenshot