Seneta Kimani Wamatangi ashinda tikiti ya UDA katika kinyang'anyiro cha ugavana Kiambu

Muhtasari

•Wamatangi alishinda katika kaunti ndogo 10 kati ya 12 za kaunti hiyo huku  akijizolea kura 68,786.

•Wainaina  alikuwa amesema yupo tayari kufanya mazungumzo na washindani wake kwa nafasi ya naibu.

Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi akijiunga na chama cha Naibu Rais William Ruto cha UDA katika uwanja wa Thika mnamo Machi 13,
Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi akijiunga na chama cha Naibu Rais William Ruto cha UDA katika uwanja wa Thika mnamo Machi 13,
Image: DPPS

Seneta wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi ndiye atakayepeperusha bendera ya UDA katika kinyang'anyiro cha ugavana wa kaunti hiyo baada ya kushinda kura ya mchujo.

Wamatangi alishinda katika kaunti ndogo 10 kati ya 12 za kaunti hiyo huku  akijizolea kura 68,786. Mbunge wa Thika Town Patrick Wainaina Wa Jungle aliibuka wa pili kwa kura 50,446.

Katika kaunti ndogo ya Githunguri, Wamatangi alipata kura 11,343 huku Wainaina akipata kura 5,870.  Huko Gatundu Kusini, Wamatangi alipata 4,318 naye Wainaina akajizolea  kura 5,090.

Wamatangi alijinyakulia kura 11,087 katika kaunti ndogo ya Limuru huku Wainaina akipata kura 5,790.

Wapiga kura 11,591 walimpigia kura Wamatangi katika kaunti ndogo ya Lari na 5, 487 wakamchagua Wainaina.

Katika eneo la Gatundu Kaskazini, Wamatangi alipata kura 5,615 naye Wainaina akapigiwa kura na watu 10,911.

Wapiga kura wachache  wa kaunti hiyo walijitokeza kushiriki katika shughuli hiyo ya Alhamisi.

Wengine waliokuwa wanatafuta tiketi ya UDA ni pamoja na aliyekuwa Gavana Ferdinand Waititu na Eric Muturi.

Hapo awali, kulikuwa na madai kwamba UDA tayari ilikuwa imemteua Wamatangi, matamshi ambayo yalitupiliwa mbali na Wainaina.

Wainaina  alikuwa amesema yupo tayari kufanya mazungumzo na washindani wake kwa nafasi ya naibu.

Wamatangi sasa atamenyana na aliyekuwa Gavana  wa kwanza wa Kiambu William Kabogo wa Tujibebe Wakenya Party, Gavana James Nyoro wa Jubilee na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria wa Chama Cha Kazi (CCK).

Wengine ni pamoja na aliyekuwa mwakilishi wa wanawake Ann Nyokabi na Juliet Kimemia (KANU).

 Wamatangi alijiunga na Naibu Rais William Ruto hivi majuzi katika mkutano wa Kenya Kwanza uliofanyika mjini Thika. Alisema alipiga hatua hiyo baada ya kushiriki mazungumzo ya kina na wapiga kura.