Raila ni kama baba kwangu, sina tatizo lolote naye- Sakaja

Muhtasari

•Sakaja amesema Raila ni kama baba kwake na kudai jukumu ambalo amelifanyia nchi kufikia mahali ilipo litabaki katika historia.

•Sakaja amesema  kuwa atajikita katika kuuza ajenda zake kwa wakazi wa Nairobi na kuhubiri siasa za itikadi.

Seneta wa Nairobi na mgombea ugavana Johnson Sakaja akizungumza katika Karen wakati wa chakula cha jioni cha Iftar mnamo Aprili 21, 2022.
Seneta wa Nairobi na mgombea ugavana Johnson Sakaja akizungumza katika Karen wakati wa chakula cha jioni cha Iftar mnamo Aprili 21, 2022.
Image: TWITTER// JOHNSON SAKAJA

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja amesema kuwa hana tatizo lolote  na mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya, Raila Odinga.

Mgombea ugavana wa Nairobi huyo kwa tikiti ya UDA amesema Raila ni kama baba  kwake na kudai jukumu ambalo amelifanyia nchi kufikia mahali ilipo litabaki katika historia.

"Raila Amollo Odinga ni kama baba kwangu. Raila ni kiongozi ambaye amekuja nyumbani kwangu kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya mwanang. Mchango  wake katika historia ya Kenya hauwezi kufutika. Ninawaheshimu," seneta huyo alisema katika Radio Citizen. Jumatano.

Sakaja alisema pia anamheshimu Rais Uhuru Kenyatta ambaye alimwamini tangu akiwa mdogo sana kuongoza chama cha kitaifa, The National Alliance.

"Namheshimu Rais Uhuru Kenyatta. Alinichagua kutoka kwa timu ya Rais Kibaki, tulianza TNA ambapo nilikuwa mwenyekiti nikiwa na umri wa miaka 26. Aliniamini na ninamshukuru."

Mgombea ugavana huyo alisisitiza kuwa hana tatizo na  yeyote kati ya viongozi  hao wawili wa muungano wa Azimio.

Aliongeza kuwa atajikita katika kuuza ajenda zake kwa wakazi wa Nairobi na kuhubiri siasa za itikadi.

"Sina suala na mtu yeyote lakini ninauza ajenda yangu, hutawahi kunisikia nikimtusi Raila Odinga au kusema lolote baya kuhusu Uhuru Kenyatta. Ninahubiri siasa safi," Sakaja alisema.

Aliongeza; "Huwezi kunisikia nikizungumza vibaya na wapinzani wangu. Nitajadili masuala tu."

Sakaja ambaye amewahi kufanya kazi na Rais Uhuru alibadili kambi na kujiunga na UDA ya Naibu Rais William Ruto.

Atachuana na mgombeaji wa kiti cha ugavana wa Azimio-OKA Polycarp Igathe ambaye anawania kiti cha mkuu wa Kaunti ya Nairobi kwa tikiti ya chama cha Jubilee.

Sakaja alichaguliwa kuwa Seneta wa Nairobi 2017 chini ya chama cha Uhuru cha Jubilee.