Sitaandaa maandamano yoyote ikiwa sitashinda urais- Ruto aapa

Muhtasari

•Ruto ameweka wazi kuwa atakubali uamuzi wa Wakenya na atakuwa ameridhika kwa kuwahi kukalia kiti cha pili cha juu zaidi nchini.

•Aliahidi kuwa  yupo tayari kumuunga mkono yule ambaye atakuwa ameshinda kiwa yeye mwenyewe atapoteza

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: EZEKIEL AMINGA

Naibu rais William Ruto ameapa kutoagiza wafuasi wake kuandamana mitaani iwapo hatashinda urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ruto ameweka wazi kuwa atakubali uamuzi wa Wakenya na atakuwa ameridhika kwa kuwahi kukalia kiti cha pili cha juu zaidi nchini.

"Mamilioni ya Wakenya hawajaweza kuwa naibu rais, nashukuru Mungu nimefika mbali hivi. Kutoka mahali nilikotoka, hapa nilipo panaridhisha. Kuwa naibu ya Kenya licha ya yote ni kitu ambacho nachukulia kama mafanikio makubwa," Ruto alisema katika mahojiano na NTV.

DP alisema Wakenya ndio watakaoamua ni nani ambaye wangependa awe rais wa tano huku akidai kuwa ameridhika na huduma ambayo ameweza kuwatolea katika kipindi cha takriban miaka tisa unusu ambacho kimepita.

Aliahidi kuwa  yupo tayari kumuunga mkono yule ambaye atakuwa ameshinda kiwa yeye mwenyewe atapoteza katika uchaguzi ujao.

"Wakiamua ni mwingine basi nitamuunga mkono ambaye atakuwa amechaguliwa na niwe sehemu ya jamii ya Kenya," Alisema.

"Naahidi kuwa sitapanga maandamano yoyote. Sitang'oa reli yoyote. Hiyo naahidi!" 

Ruto ni miongoni mwa wagombea urais wanne ambao waliidhinishwa na IEBC hivi majuzi kuwa debeni katika uchaguzi wa mwaka huu.

Atamenyana na Raila Odinga (Azimio- One Kenya), Prof George Wajackoyah (Roots Party) na David Mwaure (Agano Party).

Ni mara ya kwanza ya naibu rais kuwania kiti hicho cha juu zaidi nchini. Anatazamia kuwa rais wa tano wa Kenya kwa kutumia tikiti ya chama cha UDA na muungano wa Kenya Kwanza kwa ujumla.