Ruto adai kuwa utovu wa usalama Kerio Valley ni njama ya kumpiga kisiasa

Naibu rais alidai kuwa utovu wa usalama katika eneo la Kerio Valley ni moja wapo ya njama za serikali kumdhalilisha.

Muhtasari

• Naibu rais alidokeza kuwa kupokonywa silaha kwa NPR kulikotokea baadaye chini ya agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i na kumechangia ukosefu wa usalama Kerio Valley.

alipokuwa kwenye kampeni katika Kaunti ya Nairobi mnamo Julai 18,2022.
Kiongozi wa UDA William Ruto alipokuwa kwenye kampeni katika Kaunti ya Nairobi mnamo Julai 18,2022.
Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Naibu rais amedai kuwepo njama kubwa ya kutumia idara za serikali kumdhalilisha  na kuhujumu mipango yake kisiasa.

Naibu rais alidai kuwa utovu wa usalama katika eneo la Kerio Valley ni moja wapo ya njama za serikali kumdhalilisha.

Alidai kuwa serikali iliamua kuondoa polisi wa akiba katika eneo hilo kwa kisingizio kwamba polisi hao walikuwa watumiwe kuzua rabsha.

“Niliongoza juhudi kuleta raslimali pamoja, tukasajili zaidi ya polisi wa akiba 5000, lakini watu wengine kwa sababu zao ambazo wanajua, eti sijui walikuwa watumike kwa mambo gani, waliondoa polisi hao wote. Kilikuwa kitendo cha kusikitisha lakini kwa sababu kilikusudiwa kumwadhibu William Ruto,” Ruto alisema.

Akiongea wakati wa Mjadala wa Urais Jumanne usiku, mgombeaji urais wa Kenya Kwanza alisema hatua ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuondoa NPRs mwaka 2019 katika maeneo yanayokumbwa na mashambulizi ya majangili na wizi wa mifugo kama vile Elgeyo Marakwet na Kerio Valley ilichochewa kisiasa.

"Ifahamike kwamba watu wengi walipoteza maisha yao, ni janga la kweli, lakini hiyo ndiyo asili ya siasa zetu nchini Kenya, kwa bahati mbaya."

Ruto anahoji kuwa kwa vile alikuwa akisimamia shughuli hiyo Kerio Valley ya kukusanya rasilimali na kuhakikisha usalama umeimarishwa eneo hilo, serikali ilikosea na kuonekana kana kwamba alikuwa akifanya hivyo kibinafsi.

Kinara huyo wa UDA alidokeza kuwa kupokonywa silaha kwa NPR kulikotokea baadaye chini ya agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i na kumechangia ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

"Tulikuwa na askari wa akiba wanaokaribia 5,000, tulikuwa tumesonga mbele kutoa magari ya kivita ili kuhakikisha tunaweza kuwafuata wahalifu. Tulikuwa na mpango lakini ulisambaratishwa,” alisema.

Pia alidai kuwa kuporomoka kwa mradi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer uliogharimu mabilioni ya pesa ni hatua iliyonuia kumhujumu kisiasa kwa vile miradi hiyo iko katika eneo analotoka.

Naibu rais alisema kuwa serikali ililemaza miradi hiyo ili kuwanyima faida wafuasi wake.

Ruto alidai: "Mabwawa ya Kimwarer na Arror ilisimaishwa kwa makusudi ili kuwaadhibu wafuasi wangu."