"Nimekubali Kushindwa" - Mbunge George Theuri wa UDA, Embakasi West

Siasa si uadui bali ni ushindani wa mawazo na huduma bora kwa watu wetu - Theuri.

Muhtasari

• "Mungu awabariki nyote na ombi langu la unyenyekevu tuwe na amani na tumpe msaada na heshima MP wetu mpya" - Theuri

Mbunge wa Embakasi Magharibi George THeuri
Mbunge wa Embakasi Magharibi George THeuri
Image: MAKTABA

Mbunge wa Embakasi Magharibi George Theuri amekuwa wa hivi karibuni kukubali matokeo ya uchaguzi baada ya kushindwa na mshindani wake Mark Muriithi Mwenje.

Theuri ambaye amekuwa mbunge kwa miaka kumi alikuwa anakitetea kiti chake kwa mara ya tatu kupitia chama cha UDA na washindani wake katika eneo bunge hilo walikuwa ni Kennedy Odhiambo wa ODM na Mark Mwenje wa Jubilee.

Mwenje ambaye sasa amemshinda Theuri ni mwanawe mbunge wa zamani wa eneo hilo David Mwenje.

Theuri alikubali matokeo mapema na kuwashukuru wananchi wa Embakasi Magharibi kwa kumpa nafasi ya kuwahudumia kwa miaka kumi na pia kumtakia kila la kheri Mwenje.

“Nataka kuchukua fursa hii mapema kuwashukuru kwa dhati Jimbo zima la Embakasi west kwa kunipa nafasi ya kuwatumikia ninyi kwa miaka 10 iliyopita. Tunapoanza sura mpya niruhusu kumtakia mshindani wangu anayestahili na Mbunge mpya anayekuja wa Embakasi Magharibi Mhe Mark Mureithi Mwenje Kila la heri unapoanza enzi mpya kama Mbunge mteule,” Theuri aliandika kwenye Facebook yake.

Pia mbunge huyo anayeondoka aliwataka wananchi wa eneo hilo kujibwaga nyuma ya Mwenje ili kumpa shavu la kumrahisishia kazi anapochukua hatamu kutoka kwa Theuri.

“Kwa wafuasi wangu wote tafadhali tumuunge mkono Mh Mark Mureithi anapochukua wadhifa huo na kuipa heshima inayostahili afisi hiyo. Siasa si uadui bali ni ushindani wa mawazo na huduma bora kwa watu wetu. Katika kila shindano lazima kuwe na mshindi na mlegevu ndio maana mimi George Theuri nimekubali kushindwa na kumkabidhi kaka yangu kifungo kwa amani ili miaka 5 ijayo aitumikie Embakasi Magharibi. Mungu awabariki nyote na ombi langu la unyenyekevu tuwe na amani na tumpe msaada na heshima MP wetu mpya tunapoanza zama mpya. Hongera sana Mh Mark Mureithi Mwenje...” Theuri aliwasihi wana Embakasi.

Theuri anakuwa mwanasiasa mwingine kujitokeza wazi kukubali kushindwa baada ya awali mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kukiri kushindwa na Kimani Wamatangi katika kinyang’anyiro cha ugavana Kiambu. Wakili Cliff Ombeta pia alikubali kushindwa katika kipute cha ubunge Bonchari.