UDA yapinga agizo la mahakama kwa IEBC kutumia sajili iliyochapishwa

UDA kupitia kwa wakili Elias Mutuma walisema hawajaridhishwa na uamuzi huo.

Muhtasari

•UDA imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu kuamuru IEBC kutumia sajili iliyochapishwa kuwatambua wapiga kura katika uchaguzi wa Jumanne.

•Mutuma aliteta kuwa uadilifu wa uchaguzi mkuu unaweza kuathiriwa ikiwa sajili ya wapigakura iliyochapishwa kutumika

Viongozi wa UDA
Viongozi wa UDA
Image: Star

Chama cha UDA kimekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu kuamuru IEBC kutumia sajili iliyochapishwa kuwatambua wapiga kura katika uchaguzi wa Jumanne.

Katika maombi yaliyotolewa mbele ya mahakama ya rufaa, UDA kupitia kwa wakili Elias Mutuma walisema hawajaridhishwa na uamuzi huo.

Mutuma aliteta kuwa uadilifu wa uchaguzi mkuu huenda ukaathiriwa ikiwa sajili ya wapiga kura  itatumika.

Alisema rejista iliyochapishwa haina ulinzi wa kuimarisha uaminifu wa uchaguzi.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya Naibu Rais William Ruto kusema yuko tayari kutumia mbinu zozote ambazo tume ya uchaguzi itatumia kuwatambua wapiga kura.

Mnamo Alhamisi, mahakama ya Nairobi iliamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutumia rejista iliochapishwa kutambua wapiga kura katika uchaguzi wa Agosti.

Jaji Mugure Thande alifutilia mbali barua ambayo IEBC iliandikia Azimio, iliyoashiria kuwa watatumia vifaa vya KIEMs pekee kutambua wapiga kura.

Mahakama pia ilibainisha kuwa IEBC haikutoa taarifa yoyote kuhusu hitilafu ya teknolojia.

"Inajulikana kuwa data na vifaa kama vile simu za rununu na hata kompyuta ambazo haziitaji mtandao hupotea au kupotoshwa au kuingiliwa kupitia uhalifu na wanadamu," korti ilisema.

Mwezi uliopita, mgombea urais wa Azimio Raila Odinga alisisitiza msimamo wake kwamba sajili za wapigakura iliyochapiswa lazima zitumike katika uchaguzi wa Agosti 9.

IEBC ilikuwa imepanga kutotumia sajili zilizochapishwa siku ya upigaji kura ikisema kuwa ingetengeneza mwanya wa makosa ya uchaguzi.

Lakini Raila alisema hawataafikiana na matakwa yao ya kutaka tume kutoa sajili iliyochapishwa kama njia ya ziada ya kuwatambua wapigakura iwapo vifaa vya kielektroniki vitashindwa siku ya kupiga kura.