"Siwezi kuaibika juu ya damu yangu" Vera Sidika awasuta vikali wanaodai ataficha mtoto wake iwapo atakuwa mweusi

Muhtasari

• Vera amesema kuwa kamwe hatapata aibu juu ya mtoto ambaye amezaa mwenyewe na hatasita kupakia picha zake mitandaoni eti kwa sababu atakuwa mweusi.

•Mwanasoshalaiti huyo amedai kwamba hatua yake ya kujichumbua haimaanishi kuwa anachukia watu weusi.

•Mama huyo mtarajiwa amedai kwamba iwapo alitaka mtoto mweupe basi angechumbia mzungu ama anunue mbegu za kiume zilizotolewa kwa mzungu.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti Vera Sidika amewasuta vikali baadhi ya wanamitandao ambao wamekuwa wakimwambia awe tayari kupata mtoto mweusi kwa kuwa pia yeye alikuwa mweusi kabla ya kujichumbua.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amewajibu wanamitandao hao kwa kuwaarifu kuwa ako tayari kumpokea bintiye jinsi atakavyokuwa.

 Vera amesema kuwa kamwe hatapata aibu kwa sababu ya mtoto ambaye amezaa mwenyewe na hatasita kupakia picha zake mitandaoni eti kwa sababu atakuwa mweusi.

"Huwa napakia picha za ujauzito wangu takriban siku 3-5 kila wiki hadi mnasema mmechoka kisha mnadhani eti nitaficha mtoto wangu iwapo atakuwa mweusi.. Kweli hamko tayari. Kama mnadhani huwa najigamba na ujauzito wangu basi subiri mtoto wangu. Nitapakia!!

Instagram yangu itajaa picha zake. Mtaona mtoto huyo hadi mtakuwa mnamuota mkienda kulala. Ngojeeni tu. Siwezi kuaibika kwa sababu ya nyama na damu yangu. Haiwezekani!!  Hata atoke vipi. Huyo ni wangu kabisa" Vera aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumapili.

Mwanasoshalaiti huyo amedai kwamba hatua yake ya kujichumbua ilikuwa chaguo lake na haimaanishi kuwa anachukia watu weusi.

"Kubadili rangi ya ngozi yangu hakumaanishi kuwa nachukia watu weusi. Familia yangu yote ni weusi. Marafiki na jamaa wangu, watu ambao ninapatana nao kila siku na nakuwa mzuri kwao. Mbona mtu afikirie eti nachukia rangi nyeusi kwa sababu ya nilichokifanya? Hilo lilikuwa chaguo langu." Amedai Vera.

Mama huyo mtarajiwa amedai kwamba iwapo alitaka mtoto mweupe basi angechumbia mzungu ama anunue mbegu za kiume zilizotolewa kwa mzungu.

" Kama nilitaka mtoto mweupe basi ningechumbia mzungu ama nilipe dola kiasi kwa benki ya mbegu za kiume  na nichague mbegu za mzungu ambazo zitakuwepo ili nipate mtoto mweupe. Alaa!  Kwani nashindwa. Niko na pesa, kwa hivyo. Hata singeangalia mwafrika mara mbili" Vera amesema.

Vera ambaye kwa sasa amefunga ndoa na mwanamuziki Brown Mauzo anatarajia kupata mtoto wake wa kwanza kufikia mwisho wa mwaka huu.