"Niko na watoto kama 70!" Mhubiri mashuhuri David Ng'ang'a adai

Muhtasari

•Kwenye video ambayo imeenezwa sana mitandaoni, Ng'ang'a alisikika akifichulia waumini katika kanisa lake kwamba ana makumi ya watoto katika maeneo mbalimbali nchini.

•Mmiliki huyo wa kanisa la Neno alidai kwamba masaibu ya ndoa sio jambo geni kwa familia yake kwani  baadhi ya ndugu zake pia wamewahi  kumbwa na matatizo katika ndoa zao.

Askofu David Ng'ang'a
Askofu David Ng'ang'a
Image: IVY MUTHONI

Mhubiri mashuhuri nchini David Ng'ang'a amefichua kwamba haikuwa rahisi kwake kufunga ndoa na amepitia na kufanya mengi kabla ya kutulia na mke wake wa sasa.

Sio wazi kama mtumishi huyo wa Mungu alikuwa anapata msukumo kutoka kwa hadithi ya mfalme Solomon ama ni hali tu iliyompata lakini ufichuzi wake kwamba ana watoto zaidi ya 70 kote nchini umeacha wengi vinywa wazi.

Kwenye video ambayo imeenezwa sana mitandaoni, Ng'ang'a alisikika akifichulia waumini katika kanisa lake kwamba ana makumi ya watoto katika maeneo mbalimbali nchini.

"Mimi huwa naambia watu niko na watoto kama sabini hivi. Ukambani kama 30, Ukienda Mombasa kama ishirini na kitu hivi, huko Murang'a  na Nyandarua" Ng'anga alidai.

Ng'ang'a alidai kwamba alifanya majaribio mengi ya ndoa ila hakuwa anapata mafanikio kwani kila alipojaribu alikuwa anajipata akitengana nao baada ya muda ama kitu kingine kutokea na kufanya uhusiano ufikie kikomo.

"Mwingine alienda akiwa na ujauzito wa miezi sita. Alisema ameenda kuchua nguo lakini hakurudi" Ng'anga alisema.

Ng'anga alidai kwamba wakati mke ambaye alikuwa amefunga ndoa naye alifariki , aliamua kutafuta mke mwingine ila kwa haikuwa rahisi kutulia naye mwanzoni kwani alitoka nje ya ndoa mara 16.

"Siku moja nilijiita mkutano nikasema. Ndugu zangu wakubwa waliachwa na wake. Hao wengine nao wameaga na kuacha wake zao. Mimi  nami nimefiwa.. nilichukua nguo ya mke wangu, Tshati na picha nikapeleka kwa chumba cha maombi.Nikawekelea sadaka hapo na picha yake nikaambia Mungu, 'Mke wangu alikufa nikakuuliza nitatoa wapi kwa kuwa ubavu ulikuwa mmoja ukaniambia utanipatia. Huyu mke wangu nimemuoa rasmi na niilipa' 

Siku ingine nikachukua picha na nguo yake nikafungia kwa kijisanduku pamoja na hati ya hatimiki na nikafunga. Nikasema nimemumiliki kama hati ya hatimiki iliyokuwa pale ndani. Hadi wa leo hajawahi kutoka nje labda akienda msalani" Ng'ang'a alisema.

Mmiliki huyo wa kanisa la Neno alidai kwamba masaibu ya ndoa sio jambo geni kwa familia yake kwani  baadhi ya ndugu zake pia wamewahi  kumbwa na matatizo katika ndoa zao.

"Ndugu wangu wakubwa waliachwa na wake zao na wakaolewa kwingine na wakaendelea. Ndugu zangu wawili ambao wako chini yao walifiwa kisha wakafiwa kisha wakafa wenyewe na kuacha wake zao" Alisimulia Ng'anga.

Kwa sasa askofu huyo amefunga ndoa pamoja na Bi MercyMurugi ambaye wamebarikiwa na watoto watatu pamoja. Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2012.